WANANCHI 287 WALIPWA FIDIA KUPISHA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA RELI YA SGR TABORA - KIGOMA
August
2023
Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi ambao ardhi zao zimetwaaliwa kwaajili ya kupisha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha kwanza awamu ya pili kutoka Tabora hadi Kigoma Agosti, 2023.
Zoezi la ulipaji fidia limehusisha wananchi wapatao 287 katika vitongoji vya Fundikira, Mpigwa, Utusini na Utemini wilayani Urambo mkoani Tabora, wananchi wengine waliyolipwa fidia ni kata ya Itebula na Mganza wilayani Uvinza mkoani Kigoma ili kupisha ujenzi wa kambi ya mkandarasi, uchimbaji wa udongo kwaajili ya tuta la reli na uchimbaji wa mchanga kwaajili ya ujenzi wa kambi ya mkandarasi.
Afisa ardhi kutoka TRC Ndugu Hassan Mbaga amesema fidia iliyolipwa ni kwa mujibu wa Kanuni, Tatatibu na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Afisa mtendaji wa kata ya Kiyungi wilaya ya Urambo Bi. Biatrice Ndasa amewaambia wananchi kuwa ujenzi wa reli ya kisasa SGR unaopita katika kata ya Kiyungi utakuwa chachu ya maendeleo kwasababu wananchi watapata ajira kwa mkandarasi, wenye nyumba za kupangisha wateja wataongezeka na mama lishe biashara zao zitaimarika.
"Hizi fedha mlizolipwa mkanunue maeneo mengine " alisisitiza Bi. Beatrice.
Mmoja kati ya wananchi waliopokea fidia katika Kitongoji cha Fundikira wilaya ya Urambo mkoa wa Tabora Ndugu Laurent Kalikiti ameshukuru kupatiwa malipo ya fidia kwa wakati nakusema "sikuwahi kujenga sasa nitajenga nawashukuru sana TRC"
Shirika la Reli Tanzania linaendelea kulipa fidia kwa wananchi ambao ardhi zao zimetwaaliwa ili kupisha ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha kwanza awamu ya pili kutoka Tabora hadi Kigoma.