Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WANAFUNZI WA CHUO CHA UKAMANDA NA UNADHIMU - JWTZ WAJIONEA MAENDELEO YA MRADI WA SGR


news title here
13
October
2021

Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea ugeni kutoka kwa wanafunzi wa ukamanda na unadhimu kutoka chuo cha Jeshi la Wananchi kilichopo Arusha Tanzania kwa lengo la kuwaonesha maendeleo ya mradi wa reli ya kisasa - SGR walipotembelea ofisi za TRC na kujionea jingo la stesheni ya Dar es Salaam Oktoba 13, 2021.

Wanafunzi hao wapatao 52 wametoka katika nchi mbalimbali za ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Afrika Kusini, Nigeria, Ethiopia, Misri, Zimbabwe na Bangladeshi wakitokea katika Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kilichopo Duluti mkoani Arusha.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa dhumuni la wanafunzi hao ni kutembelea Shirika la Reli na kufahamu mipango na matazamio ya reli katika kuongeza kasi ya uchumi pamoja na kufahamu maendeleo ya ujenzi wa reli ya kisasa.

Pia ndugu Kadogosa ameeleza kuwa ziara hiyo ina umuhimu mkubwa sana kwa kuimarisha na kujenga misingi ya ulinzi katika nchi za Afrika kwa kuwaunganisha watu kutoka katika sehemu mbalimbali hali ya kuwa italeta amani na upendo baina yao bila kuangalia ukabila ama utofauti wa uraia.

“Ziara hii inakumbusha kuwa reli ni sehemu ya usalama wa nchi, sababu kiusalama reli ni mpaka nikimaanisha kuwa inatumika sana na watu kutoka nchi za jirani” alisema Ndugu Kadogosa.

Kadogosa alisistiza kuwa “Unavyowaleta watu pamoja kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakakutana na kujuana wote wanajiona ni wamoja, vitu vidodogo kama yule ni msukuma, huyu mgogo vinakua havipo, pia muunganiko wa watu unaleta amani zaidi” alisema Mkurugenzi Mkuu Ndugu Masanja Kadogosa

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Arusha Brigedia Jenerali Sylivesta Daniel amesema kuwa ujenzi wa reli ya kisasa utarahisisha usafirishaji na utachangia kiasi kikubwa sana kukuza maendeleo ya nchi.

“Naipongeza TRC kwa kujipanga vizuri katika kutekeleza sera ya viwanda Tanzania na kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri na nchi za jirani na Afika kiujumla” alisema Brigedia Jenerali Daniel.

Naye mmoja wa wanafunzi kutoka Tanzania Meja Julius Muhundi amesema ziara hiyo imetoa uelewa kwa wanafunzi kujua namna gani TRC ilivyojipanga katika kushiriki kiufasaha katika kusimamia na kujenga miundombinu ya reli katika kuleta maendeleo na kukuza pato la nchi na ukuaji wa kibiashara katika nchi za Afrika.