Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WAKUU WA MIKOA, KAGERA NA MTWARA WATEMBELEA MRADI WA UJENZI WA RELI YA KISASA


news title here
13
December
2020

Mkuu wa mkoa wa Mtwara Mhe. Gelasius Byakanwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti wakiambatana na baadhi ya vijana kutoka mikoa hiyo wametembelea jengo la Stesheni ya Reli ya Kisasa lililopo jijini Dar es Salaam, Disemba 13, 2020.

Ziara hiyo yenye lengo la kuwaonesha vijana mapinduzi makubwa yanayofanywa na serikali katika kuleta maendeleo ya kiuchumi kupitia miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameeleza lengo la ziara hiyo kwa kusema kuwa “ziara hii ni ya vijana tuliowatoa katika mikoa yetu ya Mtwara na Kagera, ni vijana wanaojishughulisha na Bodaboda, sisi tunajenga daraja kati ya vijana na serikali kwahiyo tunawaonesha miradi hii ili tuweze kuendelea kuwa na vijana ambao wapo sekta ambazo sio rasmi lakini wazalendo kwa nchi yao” alisema Mhe. Gelasius

Aidha, Mhe. Gelasius ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa kueleza kuwa “Nimeweza kujionea kazi kubwa mliyofanya, lakini hatuwezi kuwapongeza nyie watendaji bila kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jengo hili ukiliona kwa nje unaweza kusema ni dogo lakini ukiingia ndani utaona kuna vitu na sehemu nyingi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera amempongeza Mhe. Rais kwa uthubutu wa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati yenye malengo ya kukuza uchumi wa nchi

“Nimpongeze Mhe. Rais kwa uthubutu wake wa kujenga miradi hii mikubwa, tunajua mradi huu dhamira yake ni kuimarisha usafiri na usafirishaji na kuikomboa nchi yetu katika sekta ya uchumi pia tunawashukuru TRC kwa kusimamia vizuri mradi huu” alisema Mhe. Brigedia Jenerali Marco

Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji Ndugu Focus Makoye Sahani kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania ametoa shukurani kwa ugeni huo wa mkuu wa mkoa wa Kagera na Mkuu wa mkoa wa Mtwara wakiambatana na vijana wa Bodaboda na kusema kuwa ugeni huo unaleta muungano katika ushirikishwaji wa uongozi wa juu wa serikali na makundi ya jamii katika mambo ya maendeleo, pia ameeleza mchango wa vijana wa bodaboda katika sekta ya usafiri kuwa wamekuwa wakisaidia kuwahisha abiria katika miundombinu mingine ya usafiri ikiwemo reli, halikadhalika amewakaribisha watanzania kutembelea mradi wa SGR kwa lengo la kuona na kujifunza.