WAKUFUNZI KUTOKA KORAIL WAFANYA ZIARA KATIKA MRADI WA SGR DAR - MORO

September
2022
Wafanyakazi zaidi ya 30 wa Shirika la Reli Tanzania - TRC wakiambatana na wataalamu 15 kutoka Shrika la Reli la Korea - KORAIL na wafanya ziara ya siku mbili kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro Septemba 2022.
Lengo la ziara ni kujionea vituo vya reli ya kisasa na miundombinu kwa kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa mafunzo kwa vitendo uliosainiwa Julai 4 2022 mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam kati ya TRC na Shirika la Reli la Korea.
Aidha Mratibu wa Mradi wa SGR Mhandisi Faustine Kataraia ameelezea kuwa njia zitakazotumika katika mafunzo ni pamoja na njia ya darasani, vitendo yatakayotolewa ndani ya nchi na nje ya nchi. Washiriki wa mafunzo hayo ni wafanyakazi wa TRC vijana zaidi ya 30.
Naye Meneja wa Mradi kutoka Shirika la Reli la Korea Mhandisi Lee Seung Yong amesema ziara hii ni mwanzo wa mafunzo kwa vitendo kwa kujionea vituo na miundombinu ya treni ya kisasa ili waweze kutoa utaalamu wa uendeshaji wa reli ya kisasa.
Kwa upande wa watendaji wa TRC ambao watapatiwa mafunzo kwa vitendo kuhusu uendeshaji wa treni ya kisasa wamesema wapo tayari kupokea mafunzo kutoka kwa wataalamu wa Shirika la reli la Korea na wao kuwa waalimu kwa watendaji wenzao.
Ziara imehitimishwa mkoani Morogoro ambapo wataalamu kutoka Shirika la reli Korea kila mtaalamu atakuwa na watendaji wawili kutoka TRC ili kuhakiksha wanawapatia utaalamu walionao kuhusu uendeshaji wa treni ya kisasa