WAKAZI TAKRIBANI 700 KULIPWA FIDIA WILAYANI KILOSA

December
2021
Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendesha zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi takribani mia saba (700) katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro ambao ardhi zao zilitwaliwa kupisha ujenzi wa reli ya kisasa -SGR Novemba 2021.
Wananchi hao ambao ardhi zao zilitwaliwa ni kutoka vijiji vya Behewa, Mkadame, Munisagara, Mzaganza, Kikundi, Kidete, Mwasa, Kondoa, Mingo, Mbumi, Kichangani, Chanzuru, Kimamba na Kimambila wamelipwa fidia hizo baada ya ardhi zao kutwaliwa ili kupisha ujenzi miundombinu ya umeme kwa ajili ya uendeshaji wa treni za mwendokasi kwa kipande cha pili kutoka Morogoro hadi Makutupora.
Akiongea wakati wa zoezi hilo afisa jamii kutoka Shirika La Reli Tanzania Bi. Lightness Mngulu amesema kuwa zoezi hilo la ulipaji fidia ni endelevu wakati huu wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kuwa maeneo ambayo yatapitiwa na mradi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo ya umeme wananchi wanapaswa kulipwa stahiki zao kwa kuzingatia thamani ya mali zao kulingana na sheria za nchi.
“Zoezi hili ni endelevu hasa ukizingatia sasa hivi ujenzi wa Reli ya SGR unaendelea kwa hiyo wananchi watakaopitiwa na reli hii Sheria stahiki za tathmini zitafanyika na watalipwa fidia ili kupisha ujenzi huo na tunaomba tu wasiwe na wasiwasi kwa kuwa haki zao hazipotea kamwe ni suala la wao kuwa wavumilivu wakati wakusibiri kulipwa kwa kuwa lazima tathmini hizo zifuate sheria zilizo wekwa na serikali” amesema Bi Lightness Mngulu.
Aidha, Mwenyekiti wa mtaa wa Cha Behewa Kata ya Kasiki ambapo zaidi ya wakazi sabini na tisa(79) wamelipwa fidia kutokana na ardhi zao kutwaliwa, Bwana Zonobi Eusebia amesema amefurahishwa na jinsi zoezi hilo lilivyoendeshwa kijiji hapo kwani wananchi wa sehemu hiyo walipatiwa taarifa mapema kutoka kwa maafisa wa Shirika la Reli wanaosimamia zoezi hilo na hivyo iliwapa fursa wananchi hao kuandaa nyaraka muhimu zinazotakiwa ili kuweza kulipwa fidia na kulifanya zoezi la ulipaji kuwa jepesi na la uweledi.
Shirika la Reli Tanzania limekuwa likiendesha zoezi la ulipaji fidia kwa kuzingatia haki na sheria ya Nchi ya ulipaji fidia na kwa namna moja au nyingine ni dhahiri kuwa zoezi hilo limeweza kujenga imani kwa wananchi juu ya serikali yao kuwa inatimiza ahadi na kuwawezesha kuzitumia fedha wanazozipata kwenye fidia kufanya shughuli za kimendeleo na kujenga uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.