WAKAZI 500 KUPISHA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA UMEME MRADI WA SGR- KILOSA

December
2021
Shirika la Reli Tanzania- TRC linaendelea na zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya umeme ya mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha pili Morogoro- Makutupora , ambapo takribani wakazi 500 wamepatiwa hundi katika maeneo mbalimbali wilayani Kilosa- Morogoro hivi karibuni Disemba, 2021.
Maeneo hayo ni pamoja na kijiji cha Kimambila, Munisagara, Mzanganza, Kikundi, Mwasa, Kimamba, Mbumi, Mkwatani, Kibaoni, Chanzuru, Kidete, Kondoa , Magomeni, Behewa, Mlimani Boma, Mkadage, Mingo pamoja na Kijiji cha Kichangani.
Afisa ardhi kutoka TRC Bw. Seprine Rwegerela amesema kuwa wananchi wanaonyesha ushirikiano kwa kujitokeza kwa wingi kupokea stahiki zao na pia kufurahishwa sana na maendeleo ya mradi wa SGR ambayo hadi sasa yamefikia katika hatua nzuri kwa kipande cha pili cha Morogoro- Makutupora.
“Wananchi wengi wanaonyesha kufurahishwa na maendeleo ya mradi SGR “ alisema Bw. Seprine.
Pia Bw. Seprine ameeleza kuwa wananchi wamepata fursa ya kupewa ulewa jinsi ya kutumia malipo hayo katika mambo muhimu yatakayo waletea maendeleo kwenye jamii zao kama vile kuwekeza katika kukuza kilimo , biashara pamoja na kujenga nyumba za kisasa pasi na kutumia malipo hayo bila faida ya baadae.
“Tunafanya kazi kubwa kuelimisha wananchi kutumia malipo yao kiufasaha ili majuto yasijitokeze, maendeleo yanatakiwa kuwepo nchini “ alisema Bw. Seprine.
Naye mwenyekiti wa kijiji cha Kimambila- Kilosa Bw. Saidi Manga amesema kuwa mradi wa SGR umebadilisha taswira ya maeneo mbalimbali katika wilaya ya Kilosa ikiwemo kuwepo kwa nyumba za kisasa , nishati ya umeme, ongezeko la biashara na ajira , kupanda thamani ya ardhi ambapo ukuaji wa uchumi kwa wananchi umekua mkubwa.
“Wananchi wakipata maendelea bila shaka na mapato ya nchi yanaongezeka katika ulipaji wa kodi zinazotokana na wananchi “ alieleza Bw. Manga.
Vilevile mkazi wa kijiji cha Kimambila Bw. Athumani Rajabu ameishukuru serikali kwa kujenga mradi wa kimkakati ambao unaleta manufaa kwenye jamii mbalimbali kuweza kujikwamua kiuchumi na kuwa na mawazo mapya ya maendeleo.
“ Wananchi wanapaswa kuonyesha ushirikiano na kutoa maeneo yao kwa moyo mkunjufu , haya maendeleo ni ya nchi nzima sababu serikali ni kwaajili ya wananchi” alisema Bw. Rajab.