WAJUMBE WA BARAZA LA WAFANYAKAZI TRC WATEMBELEA MRADI WA UJENZI YA RELI YA KISASA –SGR KIPANDE CHA DAR – MORO
February
2020
Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania – TRC watembelea mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR kipande cha Dar es Salaam – Morogoro tarehe 17 Februari 2020.
Wajumbe wamefanya ziara hiyo kwa lengo la kuona maendeleo ya ujenzi ya Reli ya Kisasa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro ambacho ujenzi wake umefika zaidi ya asilimia 73, ikiwa ni utaratibu wa Baraza hilo kutembelea Miradi ya Shirika kuona kasi ya utekelezaji wake pindi unapoisha mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ambalo lilifanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia Februari 15 – 16, 2020 katika ukumbi wa ‘Fire and Safety’ Bandari jijini Dar es Salaam.
Wajumbe walitembelea katika stesheni mbalimbali za reli ya kisasa, kuanzia stesheni ya Dar es salaam ambao ujenzi wake umefika asilimia 65, stesheni ya Pugu asilimia 85 na stesheni ya Soga asilima 90, sambamba na ujenzi wa Stesheni pia wamepata fursa ya kuona kazi nyingine za ujenzi zikiwa mbioni kukamilika.
Wakiwa katika ziara wajumbe waliweza kupata taarifa kamili kuhusu maendeleo ya mradi katika kambi kubwa ya ujenzi wa reli ya kisasa iliyopo Soga wilaya ya Kibaha mkoani Pwani na kuona kiwanda cha kutengeneza mataruma ya reli ya kisasa ambacho huzalisha mataruma 1500 kwa siku huku wataalamu wanaofanya shughuli hiyo wengi wao wakiwa ni wazawa.
Akiongea katika ziara hiyo Kaimu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Wafanyakazi Shirika la Reli – TRC Ndugu Amina Lumuli kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi TRC ameushukuru uongozi, Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa jitihada zinazofanywa na Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu Mradi huu wa Reli ya Kisasa.
“Tumekuwa na ziara ya mafanikio, Baraza la Wafanyakazi ni wawakilishi wa wafanyakazi tulianza mkutano wa Baraza siku ya Jumamosi lengo kuu likiwa ni kupitisha bajeti ya mwaka 2020/2021 pamoja na kuangalia mustakabali mzima wa taasisi, leo tunahitimisha Baraza kwa kutembelea Mradi huu unaosimamiwa na Shirika la Reli nchini” alisema Amina
Kwa upande wake Mhandisi Mipango Ndugu Enice Eryilmaz kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Yapi Merkezi amesifu Tanzania kuwa kama ‘Paradise’ kwa maana ni nchi ambayo hajawahi kukutana nayo, ina watu wachapakazi na wenye maarifa na elimu ya kutosha kuweza kufanya kazi katika Miradi mikubwa ukilinganisha na nchi ambazo wamewahi kufanya kazi kwani huwalazimu kuleta wataalamu kutoka nje kwa ajili ya kuwasimamia wataalamu wazawa ambapo ni gharama zaidi, pia Mhandisi Enice amesema kuwa hawakutegemea kupata nguvu kazi ya wataalam wazawa kwa idadi kubwa kwa sababu nchi zingine hufanya asilimia 50 kwa 50 ila kwa Tanzania wamepata asilimia 53.3 ya wafanyakazi watanzania hivyo ni jambo la kujivunia kwa Tanzania.
Aidha Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Ndugu Edwin Kalisa amesema Mradi huu ni wa Watanzania, wajumbe wa Baraza ni vizuri watembelee kwani ni mabalozi wa kusambaza habari kwa wafanyakazi wa Shirika zima kuhusu yanayoendelea kwenye mradi ni ngumu kuwaleta wafanyakazi wote kwa pamoja kuja kuona mradi hivyo Wajumbe wawe mabalozi wa kufikisha haya, ameongeza kuwa Baraza la Wafanyakazi limesitishwa hivyo wajumbe wataweza kurudi katika maeneo yao ya kazi baada ya kuweka maadhimio na kutekeleza yale yaliyoyapangwa ili kuweza kukamilisha mradi huu.
Mmmoja wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi TRC Ndugu Focus Sahani amelishukuru Shirika kwa ziara hiyo kwani ni mafunzo tosha na watakuwa mabalozi wazuri kusambaza habari za mradi kwa wafanyakazi, amesisitiza kuwa kinachotakiwa kwa wafanyakazi ni kujiandaa ili kuweza kuisimamia reli mpya ya kisasa pindi wakandarasi watakapomaliza ujenzi huo hivyo amewataka wafanyakazi wawe na moyo wa kujifunza kwa makini ili kupata uelewa wa vitu vipya vinavyokuja.