TRC, TCB WAZINDUA KADI YA MALIPO YA TIKETI USAFIRI WA SGR

October
2025
Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa ushirikiano na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) limezindua rasmi kadi ya malipo ya tiketi ya SGR iitwayo TRC Prepaid Card katika hafla fupi iliyofanyika katika jengo la stesheni ya SGR ya John Pombe Magufuli iliyopo jijini Dar es Salaam Oktoba 10,2025.
Akiongea kwenye hafla hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara TRC Bw. Fredrick Masawe, alisema kuwa dhamira ya TRC ni kuhakikisha kila msafiri anafurahia ufanisi, usalama na kuhamasika katika kila hatua ya safari kwa kufanya malipo kwa urahisi kupitia kadi hiyo.
“Mabadiliko ya kidijitali yanaendelea kuleta umuhimu wa kadi hii, hivyo TRC kushirikiana na TCB tumeona tusibaki nyuma kutokana na Dunia ya sasa inavyoendelea kubuni teknolojia mpya” alisema Bw. Masawe.
Aidha Bw. Masawe amesema kuwa kupitia kadi hiyo italeta ufanisi wa kuweka fedha kwa wepesi na mteja kuweza kufanya malipo ya tiketi pasi na kufika stesheni.
“Kadi hii ya malipo itatolewa bila ya malipo ya aina yeyote katika vituo vyote vya stesheni halikadhalika itapunguza changamoto ya msongamano wa kukata tiketi maeneo ya stesheni na kufanya malipo yawe kwa urahisi” aliongezea Bw. Masawe.
Katika hatua nyingine, Bw. Masawe alielezea umuhimu wa kadi hiyo kuwa itaruhusu kuweka fedha na kutoa kwa usalama na wepesi wa matumizi na pia kutumika kwenye mashine ya kutokea pesa(ATM) za Umoja Switch hata baada ya safari.
Wakati huo huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCB Bw. Jema Msuya, amesema kuwa kadi hiyo pia itatumika katika maeneo mbalimbali kama kwenye migahawa, hoteli na kumuongeza urahisi mtumiaji.
“Mtumiaji wa kadi hii kadiri atakavyoitumia atapata pointi ambazo zitakuwa kama zawadi kwenye miamala atakayokuwa akiifanya na pia kadi hii itapatikana kwenye mitandao yote ya simu na pia kupitia TCB Mobile App” alieleza Bw. Msuya.