Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WAJUMBE HALMASHAURI KUU CCM WARIDHISHWA MAENDELEO YA MRADI WA SGR


news title here
06
December
2022

Wenyeviti pamoja na wajumbe kutoka visiwani Zanzibar na Bara wa Halmashauri kuu ya Taifa Chama Cha Mapinduzi - CCM watembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kwa kutumia treni ya mkandarasi kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, Disemba 05, 2022.

Ziara hiyo imeongozwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM. Prof. Mbarawa alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi kimekua washauri wakuu katika ujenzi wa reli ya kisasa kwa kutoa mawazo chanya yaliyopeleka kuendelea kukuza miundombinu ya reli nchini.

“Reli hii ilikua imebuniwa kwa mwendo wa kilomita 120 kwa saa pia ilikua sio ya umeme lakini CCM iliona mbali na kutushauri kuongeza mwendokasi wa kilometa 160 kwa saa pamoja na kuwa na treni itakayotumia umeme” alisema Mhe. Prof. Mbarawa .

Aidha, Prof. Mbarawa alieleza kuwa SGR ni mradi wa kimkakati ambao unatekelezwa na serikali kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambapo kazi kubwa inaendelea kufanyika katika vipande vyote kutoka Dar es Salaam – Mwanza huku vipande vingine ikiwemo vya kuunganisha Tanzania nan chi jirani vikiwa katika mkakati.

“Mwakani tutasaini mkataba kwaajili ya ujenzi wa reli ya kisasa kuunganisha Tanzania na Burundi” alisema Prof. Mbarawa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa alisema kuwa ugeni huo unatoa hamasa kwa TRC kwakuwa wajumbe wametembelea mradi huo na wameridhishwa na walichokiona katika.

“Wenyeviti wa CCM nchi nzima Mikoa yote 32 wameambatana na wajumbe wa NEC bara na visiwani wanapokuja kutembelea mradi na kuridhika kwa kuona maendeleo ya mradi hii ni hatua nzuri ya kujivunia” alisema Ndugu Kadogosa.

Pia Mwenyekiti wa CCM kutoka mkoani Singida Bi. Martha Mlata alisema kuwa ujenzi wa reli ya kisasa utaleta manufaa ya kusafirisha bidhaa na mazao katika mkoa wa Singida ikiwemo zao la alizeti, vitunguu pamoja na mifugo vilevile itanufaisha mikoa mingine na kufanya pato la taifa liendelee kukua.

“Sisi tulioona ndio tutakua mabalozi pia kwa vijana wetu walioshiriki kwa asilimia kubwa tunaamini wamejifunza mambo mengi hivyo tutaendelea kujenga miundombinu yetu kupitia nguvu kazi ya taifa letu“ alisema Bi. Martha.

Hata hivyo Mwenyekiti wa CCM kutoka mkoani Tabora Bw. Hassan Mwakasuvi ameipongeza serikali kupitia TRC kwa kuendelea kusimamia vema mradi huu kwani utakua chachu ya utalii wa ndani kupitia maeneo mengi zikiwemo stesheni zote za SGR.

“Hii ni dhamana kwaajili ya taifa letu hivyo tunapaswa tuitunze” alisema Bw. Hassan.

SGR ni moja kati ya miradi ya kimkakati ambayo Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuitekeleza, mradi uko mbioni kuanza uendeshaji kwa kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro ambapo kimefikia zaidi ya asilimia 97.