Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI WATEMBELEA MRADI WA SGR


news title here
16
February
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea ugeni wa Wahariri wa vyombo vya habari nchini kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro hivi karibuni Februari, 2023.

Ziara hiyo ya Wahariri iliyofanyika kuanzia stesheni ya SGR Dar es Salaam hadi Soga mkoani Pwani ambapo wamepata fursa ya kufahamu mambo mbalimbali yanayohusu mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa ameeleza kuwa miundombinu ya reli ikiwemo SGR itakua ya kisasa yenye ubora ambayo itakuza maendeleo ya nchi na wananchi.

“Tunajenga mradi huu ambao ni wa kisasa zaidi hivyo wahariri watatuwakilisha vyema kupitia vyombo vyao vya habari” alisema Bw. Msigwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu kutoka TRC Ndugu Masanja Kadogosa alisema kuwa nchi ya Tanzania imepakana na nchi zaidi ya saba hivyo lengo la mradi huo ni kuwekeza katika sekta ya usafirishaji ikiwemo wa abiria na mizigo ili kukuza nchi kibiashara.

“Reli ni uwekezaji mkubwa sana katika taifa, wafanyabiashara watabeba mzigo mingi sana kwa wakati mmoja” alisema Ndugu Kadogosa.

Mhariri wa Gazeti la Nipashe Bw. Epson Luhwagu alisema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya mafunzo ambayo pia itawafanya wahariri kupata taarifa sahihi za mradi wa SGR.

“Tunawashukuru sana TRC kwa kutukaribisha kufanya ziara hii ambayo italeta tija katika tasnia ya habari kwa ujumla” alisema Bw. Luhwagu.

Ziara hiyo ya wahariri iliambatana na Semina siku ya Jumanne Februari 14, 2023 katika ukumbi wa City Garden Gerezani jijini Dar es Salaam.