WAFANYAKAZI TRC WASHIRIKI MAFUNZO MAALUMU YA AJIRA NA MAZINGIRA YA KAZI KATIKA UTEKELEZAJI MIRADI

February
2022
Wafanyakazi wa Idara mbalimbali kutoka Shirika la Reli Tanzania - TRC hivi karibuni wameshiriki semina ya mafunzo ya uelewa kuhusu utekelezaji wa Sheria na Sera mbalimbali zilizoainishwa kwenye mkataba wa kimataifa wa ajira na mazingira ya kazi wa Shirika la Fedha Duniani (WB) wa mwaka 2012 kuhusiana na utekelezaji wa Miradi, Dar es Salaam Februari 25, 2022.
Semina hiyo ya siku mbili imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Holiday Inn jijini Dar Es Salaam, ikilenga kuwajengea uwezo wafanyakazi juu ya uelewa katika masuala yanayohusu mahusiano kati ya TRC na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya reli hapa nchini kwenye masuala tambuzi ya Ajira na Mazingira ya kazi ya wafanyakazi kwa kufuata Sheria ya kimataifa ya kazi na ajira kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Shirika la Fedha Duniani (WB ) na kitengo maalumu kinachosimamia mikataba hiyo IFC (International Finance Corporation) juu ya utekelezaji wa miradi.
Miongoni mwa masuala yalioanishwa katika mafunzo hayo kuhusu utekelezaji wa Sheria hizo ni ssalama kazini, ajira, ufanisi na upatikanaji wa vitendea kazi, faida za miradi kwenye jamii, utatuaji wa migogoro ya ardhi katika miradi inayoendelea, ulinzi wa viumbe hai katika mazingira ya ujenzi unapofanyika na uzingatiaji wa tamaduni husika ambapo miradi hiyo inatekelezwa.
Akizungumza wakati wa semina hiyo Mkuu wa kitengo cha Mazingira na Jamii kutoka Shirika la Reli Tanzania Bi. Catherine Mroso amesema semina hiyo inaazimia kujenga uelewa na uhusiano mzuri kati ya wafanyakazi wa TRC na wakandarasi wa miradi ya reli katika namna bora ya usimamizi wa ajira na rasilimali watu ili kuleta ufanisi katika utendaji.
“Mafunzo haya ni maalumu kwaajili ya kujenga uelewa wa kimahusiano kati ya wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania na Mkandarasi katika namna bora ya kuongeza ufanisi kwa kusimamia wafanyakazi na mzingira ya kiutendaji na hususani kwa idara ya rasilimali watu itaongeza uwezo wa usimamizi wa sheria za ajira hivyo kuimarisha utendaji” alisema Bi. Catherine Mroso.
Edymango Gowele, mmoja ya mshiriki kutoka Idara ya Mipango na Uwekezaji TRC amesema kuwa mafunzo hayo yatawezesha wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania kufanya majukumu yao kwa kufuata sheria na vilevile kila mmoja miongoni mwa wafanyakazi wa Shirika hilo katika nafasi yake ya kiutendaji atatekeleza majukumu kwa weledi na ufanisi ili kukidhi matakwa ya wafanyakazi na jamii kwa ujumla.
Shirika la Reli ambalo limepewa dhamana ya usimamizi wa ujenzi na maendeleo ya miundombinu ya reli litahakikisha uzingatiaji wa Sheria za msingi katika kutekeleza miradi hiyo inafuatwa kwa kuzingatia Sheria zilizoainishwa katika vifungu mbalimbali vya kitaifa na kimmataifa ili kulinda maslahi ya wafanyakazi .