Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

WAFANYAKAZI TRC WAADHIMISHA SIKU YA WAFANYAKAZI MEI MOSI


news title here
02
May
2021

Wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania – TRC washiriki Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi iliyoadhimishwa kitaifa katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza Mei 01, 2021.

Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani hufanyika Mei 01 kila mwaka Duniani kote kwa lengo la kuwakutanisha wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka 2021 ni “Maslahi Bora, Mishahara Juu” huku Mgeni Rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Sambamba na Ushiriki wa TRC katika maadhimisho hayo kitaifa, wafanyakazi wa TRC katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Dodoma, na Tabora nao wameadhimisha sherehe hizo kwa kufanya maandamano katika maeneo yao.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amekabidhi Hundi kama zawadi kwa Wafanyakazi Bora na Hodari wa Shirika kwa mwaka 2021, ambapo Mfanyakazi Bora Bwana Mommy Mwakyusa amepata Shilingi Milioni Tatu akifuatiwa na Bwana Bura Maringa aliyepata nafasi ya Mfanyakazi Hodari na kukabidhiwa Shilingi Milioni Mbili huku washindi wengine Sita kutoka Makao Makuu, Kanda ya Dar es Salaam, Tanga na Tabora wakipata ya Shilingi 1,500,000 kila mmoja.

“Leo Mhe. Rais amekabidhi zawadi kwa Wafanyakazi Bora lakini pia sisi tumekutana hapa kama wafanyakazi kupongezana kwa baadhi ya wafanyakazi waliofanya vizuri na nimekabidhi pia zawadi za Shilingi 2,000,000 kwa mfanyakazi Hodari, na Shilingi 1,500,000 kwa wafanyakazi Hodari wengine sita pia tumekutana kujadili Mustakabali wa Shirika letu” alisema Kadogosa

Mkurugenzi Mkuu wa TRC amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhudhuria Sherehe za Mei Mosi na ameongeza kuwa mambo ambayo Mhe. Rais ameyazungumza yamewagusa wafanyakazi wa Shirika hilo ikiwemo kupunguza Kodi katika Makato ya Mishahara na Mikopo ya vyuo vikuu lakini pia ameahidi kuhakikisha Shirika linaongeza tija katika uzalishaji ili kuongeza mapato kama alivyoagiza Mhe. Rais.

Mmoja wa wafanyakazi Bora Bi. Regina Singano ameeleza hisia zake mara baada ya kupokea zawadi yake “Nimefurahi sana kuwa mfanyakazi Hodari namshukuru Mwenyezi Mungu kwani bila yeye, bila wafanyakazi wenzangu nisingeweza kuwa mfanyakazi hodari, naishukuru ofisi yangu nalishukuru Shirika la Reli”

Naye Awadhi Mashanga, Muongoza Treni Mwanza amesema kuwa amefarijika na ameona kuwa taasisi imemtendea haki kwa zawadi iliyompatia lakini pia anatarajia zawadi hizo zitakuwa kama motisha kwa wafanyakazi wengine waweze kuchapa kazi zaidi.