Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WADAU WA VIPINDI VYA ELIMU KWA UMMA WATEMBELEA MRADI WA SGR


news title here
23
February
2023

Washiriki wa mkutano wa 107 wa waandaaji wa vipindi vya elimu kwa umma wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania – TBC Dkt. Ayub Rioba Chacha watembelelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kuanzia Morogoro hadi Kilosa, Februari 22, 2023.

Ziara imehusisha wanahabari na waandaaji wa vipindi vya elimu kwa umma kutoka Taasisi za Serikali na Binafsi kwa lengo la kujifunza na kuona maendelea ya mradi wa SGR. Mkutano wa mwaka 2023 umeambatana na kaulimbiu isemayo “VYOMBO VYA HABARI NI CHACHU YA MIRADI YA MAENDELEO”

“TBC imeandaa haya mafunzo na huu ni mkutano wa 107 na kaulimbiu kwa mwaka huu ni VYOMBO VYA HABARI NI CHACHU YA MIRADI YA MAENDELEO na ndiyo maana tukaamua tutembelee mradi wa SGR kwa sababu ni mradiw a kujivunia” alisema Dkt. Ryoba

Wadau walipata fursa ya kutembelea jengo la stesheni ya SGR mkoani Morogoro, kituo cha umeme namba tano kilichopo Mkata na Handaki refu katika mradi linalopatikana Kilosa mkoani Morogoro ambapo wahandisi kutoka Shirika la Reli Tanzania – TRC waliwapatia maelezo ya kina kuhusu miundombinu ya kisasa inayopatikana katika mradi wa kimkakati wa SGR.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano Bi. Jamila Mbarouk amesema kuwa TRC inashukuru kupata fursa ya kutoa elimu katika mkutano wa wanahabari na kutoa fursa ya kutembelea mradi wa SGR kutoka Morogoro hadi Kilosa. Kupitia ziara hii wanahabariw atakuwa mabalozi wazuri kuisemea Serikali, kwasababu ili Serikali iweze kuaminika na kukubalika ni lazima wananchi wapate taarifa sahihi na kwa wakati kupitia wanahabari ambao ni watu sahihi wa kuisemea Serikali.

Mshiriki kutoka Zanzibar Bi. Nafisa Ally, Mkuu wa kitengo cha Habari Ofisi ya jiji la Zanzibar amesema kuwa “ni jambo jema sana kutembelea mradi, naishukuru taasisi ya TBC kwa kuandaa mafunzo na kutupatia fursa kama wanahabari kuja kujionea kwa macho mradi huu wa kimkakati na kwakweli tutakuwa mabalozi wazuri wa wenzetu kwasababu ni fursa pekee tuliyoipata”

Bwana Suleimani Burenga, kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ameipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya katika kuboresha miundombinu kwakuwa miradi ni mikubwa na inachukua gharama kubwa lakini pamoja na mazingira hayo vitu vimefanyika kwaajili ya kujenga uchumi wa aifa na watu wake.