Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​WABUNGE WASHIRIKI SEMINA YA UELEWA KUHUSU MRADI WA SGR


news title here
04
May
2024

Wizara ya Uchukuzi kupitia Shirka la Reli Tanzania – TRC limefanya semina elekezi kwa Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR unaoendelea, semina imefanyika katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, Mei 2023.

Lengo la Semina ni kuwajengea uelewa wa pamoja wabunge kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa unaoendelea awamu ya kwanza Dar es Salaam – Mwanza, awamu ya pili Tabora – Kigoma pamoja na vipande va Mtwara – Mbambabay na Uvinza – Msongati.

Semina iliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Moshi Selemani Kakoso ambapo Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania – TRC walitoa ufafanuzi kuhusu mambo mbalimbali na kujibu maswali ya wabunge.

Mhe. Kakoso amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazofanya kutenga fedha zaidi ya Trilioni 10 kutekeleza mradi pia amempongeza Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa kwa kuhakiksha miradi inakamilika kupitia jitihada za kuhakikisha Fedha kwaajili ya mradi zinapatikana.

“Mliowapa dhamana (Shirika la Reli) wamefanya kazi kubwa kwenye usimamizi na lipo jambo kubwa limefanywa na menejimenti ya TRC wabunge hamlifahamu, kwenye mikataba walioingia na wakandarasi suala la gharama wamelizingatia kiasi kwamba hata mradi ukiongezeka gharama mkataba utabaki vilevile” aliongeza Mhe. Kakoso

Aidha, akifunga Semina Mhe. Kakoso ameiomba Serikali ikamilishe hatua za kupata wawekezaji kwaajili ya kuanza mradi wa reli ya Mtwara kwenda Mbamba bay kupitia Liganga na Mchuchuma, ameiomba Serikali iweke mkakati wa kuhakikisha miundombinu iliyojengwa kwa gharama kubwa inalindwa pia Serikali ihakikishe wakandarasi wadogo wanaofanya kazi kwenye mradi wanalipwa pamoja na kuwekeza kwenye rasilimali watu

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Makame Mbarawa ametolea ufafanuzi kuhusu suala la nauli za treni ya mwendokasi kuwa TRC haina mamlaka ya kutangaza nauli isipokuwa ni suala la kisheria hivyo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini – LATRA inaendelea na mchakato na nauli ziatatangazwa ambapo kila mwananchi ataweza kumudu gharama za kusafiri na treni ya mwendokasi.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa alitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa SGR pamoja na maandalizi ya kuanza utoaji huduma mapema mwezi Julai 2024. Kadogosa alieleza hatua iliyofikiwa kwaajili ya kuanza ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa kutoka Mtwara hadi Mbamba bay na Uvinza Msongati.

Bunge la bajeti kwaajili ya mwaka 2024/25 linaendelea ambapo Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi inatarajia kusomwa Bungeni tarehe 6 Mei 2024 jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya uwasilishwaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25 huku mradi wa SGR ukichukua kiasi kikubwa cha bajeti ya Wizara na Serikali kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea katika sekta ya reli nchini.