WANANCHI WATWALIWA MAENEO YAO KWAAJILI YA KUCHIMBA VIFUSI MRADI WA SGR

October
2022
Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la malipo ya fidia kwa wananchi ili kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha pili Morogoro- Makutupora kwaajili ya maeneo ya kuchimba vifusi lililofanyika wilaya ya Dodoma mjini pamoja na wilaya ya Bahi mkoani Dodoma hivi karibuni Oktoba, 2022.
Maeneo yaliyotwaliwa ili kupisha mradi huo wa ujenzi wa reli ya kisasa ni pamoja na kijiji cha Chanhumba, mtaa wa Maganga uliopo Dodoma mjini, Bahi Mapinga na kijiji cha Mapinduzi kilichopo wilaya ya Bahi.
Afisa ardhi kutoka TRC Bw. Ramadhani Mfikilwa ameeleza kuwa wananchi wanaendelea kunufaika na mradi huo kwakua maeneo yanaendelea kutwaliwa ili kukamilsha shughuli mbalimbali za ujenzi ikiwemo maeneo ya kuchimba vifusi, maeneo ya kutupia udongo usiofaa, pamoja maeneo ya njia ya umeme.
“Mradi huu wa SGR ni mradi mkubwa hivyo unahitaji maeneo mengi yatakayoweza kurahisisha mchakato mzima wa ujenzi” alisema Bw. Ramadhani.
Aidha, Bw. Ramadhani alitoa rai kwa wananchi kuhakikisha kuwa na hati miliki za maeneo yao ili kuepusha mkanganyiko pindi inapohitajika kupatiwa malipo ya fidia kwasababu ya kukosa nyaraka husika za eneo husika lililotwaliwa.
“Tumeona watu wengi wanasimama katika eneo lakini hati miliki inatambulisha jina tofauti au nyaraka zinakuwa pungufu hivyo kuwalazimu kwenda kufuatilia upya katika Ofisi za ardhi jiji” alisisitiza kuwa "wananchi anatakiwa awe na utambulisho sahihi kwenye nyaraka pamoja na kitambulisho cha mpiga kura ama cha taifa” alisema Bw. Ramadhani.
Naye Mwenyekiti kutoka katika kijiji cha Mapinduzi Bw. Joseph Mkwawa amesema kuwa elimu ya uelewa kuhusu miradi ya nchi iendelee kutolewa kwa wananchi mara kwa mara ili kuwakumbusha hasa wanakijiji kuwa dunia inazidi kubadilika na maeneo yanazidi kukua kutokana na maendeleo ya nchi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo mradi huo wa SGR.
“Watu wa vijijini wengi hawana elimu hivyo wanaanza kuamka kupitia miradi mikubwa ndio wanajua kumbe kuna benki, au nyaraka ni lazima wawenazo hivyo kiukweli mradi unatusaidia na sisi kuwa wa kisasa” alisema Bw. Mkwawa.
Mwananchi kutoka katika kijiji cha Mapinduzi Bi. Matha Hussein ameishukuru serikali kupitia TRC kwa kuleta maendeleo vijijini vilevile kuwapatia wananchi malipo yao ya fidia ikiwa ni chachu kwa wananchi kufanya mambo mengine ya kimaendeleo katika vijiji vyao.
TRC inaendelea na zoezi hilo la malipo ya fidia katika maeneo ambayo yametwaliwa ili kupisha mradi wa SGR pamoja na wananchi ambao walikutwa na kasoro mbalimbali za nyaraka zao wakati wa malipo ya awali.