Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​VIONGOZI WA CHAMA CHA RPF – INKOTANYI NCHINI RWANDA WATEMBELEA SGR


news title here
02
July
2023

Shirika la Reli Tanzania – TRC limetembelewa na viongozi wa Chama Tawala cha Rwanda RPF – Inkotanyi wakiongozwa na Katibu Mkuu Ndugu Wellars Gasamagera, viongozi hawa wametembelea ujenzi wa mradi wa reli yenye kiwango cha kimataifa (SGR) kipande cha kwanza Dar es Salaam – Morogoro katika jengo la stesheni ya SGR jijini Dar es Salaam tarehe 01 Julai 2023.

Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kadogosa ameushukuru uongozi wa CCM chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha viongozi wa RPF kutembelea TRC ili kuona maendeleo ya ujenzi wa SGR na shughuli zote zinazofanywa na TRC.

“Mizigo mingi ya Rwanda hupita katika bandari ya Dar es Salaam kwahiyo ujenzi wa SGR utakapokamilika itawarahisishia wafanyabiashara wa Rwanda kwasababu mizigo yao watakua wanachukulia Bandari kavu ya Isaka kupitia usafiri wa reli ya kisasa kutoka bandari ya Dar es salaam hadi Isaka, pia mipango ya Serikali ni kujenga SGR kutoka Isaka hadi Lusumo kwa kuunganisha na Rwanda hadi Kigali” amesema Masanja Kadogosa.

Katibu Mkuu wa RPF Ndugu Wellars Gasamagera amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia maendeleo ya ujenzi wa reli ya SGR na kujifunza namna itakavyofanya kazi, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi wa SGR kwani utaleta maendeleo katika usafirishaji ndani na nje ya nchi.

“Kwa baadaye mradi wa SGR utaunganisha Tanzania na Rwanda na sisi tupo tayari kuupokea nchini Rwanda” amesema Gasamagera.

Naye Katibu Halmashauri kuu ya Taifa Oganaizesheni CCM Ndugu Issa Haji Ussi amesema mradi umefika pazuri na pindi huduma ya usafirishaji itakapoanza itarahisisha usafirishaji wa mizigo pamoja na abiria nchini.

“SGR inaenda kua kiunganishi na nchi jirani zikiwemo Congo na Rwanda kupitia usafirishaji wa mizigo kutoka bandari kuu ya Dar es Salaam” ameongeza Issa Ussi.

TRC imepewa dhamana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusimamia ujenzi wa reli yenye kiwango cha kimataifa ( SGR) katika awamu ya kwanza na mpaka sasa ujenzi umefanyika na unaendelea katika vipande vitano ambavyo ni Dar es Salaam - Morogoro , Morogoro - Makutupora , Makutupora - Tabora , Tabora - Isaka na Isaka Mwanza na ujenzi wa awamu ya pili Tabora - Kigoma.