Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​VICHWA 3 VYA TRENI YA UMEME VYAWASILI NA MABEHEWA 27


news title here
30
December
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea Vichwa vipya 3 vya treni za umeme na Mabehewa mapya ya abiria 27 kwa ajili ya reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR katika Bandari ya Dar es Salaam Disemba 30, 2023.

Vichwa vitatu (3) vya treni ya umeme vimeundwa na kampuni ya Hyundai Rotem na mabehewa ya abiria ishirini na saba (27) yaliundwa na kampuni ya 'Sung Shin Rolling Stock Technology' (SSRST) kutoka nchini Korea Kusini.

Kaimu Mkurugenzi TRC Mhandisi Machibya M. Shiwa alisema kuwa vifaa vilivyopokelewa ni muendelezo wa vifaa ambavyo vinaendelea kuundwa nchini Korea Kusini pamoja na nchi zingine kwa ajili ya uendeshaji wa SGR.

“Tumepokea vichwa vitatu(3) vya treni za umeme hivyo jumla ya vichwa tulivyopokea hadi sasa ni vinne kati ya vichwa kumi na saba (17) vinavyoundwa na kampuni ya Hyundai Rotem kutoka Korea Kusini” alisema Mhandisi Machibya.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Machibya alieleza kuwa jumla ya mabehewa yaliyopokelewa hadi sasa ni 56 kati ya mabehewa 59 ya abiria kutoka katika kampuni ya SSRST ya nchini Korea Kusini.

“Katika bachi tuliyoipokea leo ina mabehewa ya daraja la biashara (business class) kumi na tatu (13) na mabehewa ya daraja la uchumi (economy class) kumi na nne(14)” alisema Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Machibya.

Aidha, aliongezea kuwa mabehewa hayo 59 yakikamilika kutakuwa na behewa moja ambalo ni maalumu kwa kiongozi wa nchi (presidential coach).

Hata hivyo kaimu Mkurugenzi, Mhandisi Machibya ameeleza kuwa mnamo mwaka 2024 TRC itaanza kupokea treni 10 za kisasa Electrical Multiple Units (EMU).

“Seti ya kwanza (1) itapokelewa mwezi Machi, seti 2 zitapokelewa Mei, Juni Seti 2, Julai seti 2, Septemba seti 2 na seti ya mwisho itapokelewa Oktoba 2024 ambapo seti moja ya treni hiyo itakua na uwezo wa kubeba watu 640” aliongezea Mhandisi Machibya.

Vichwa vilivyopokelewa vina uwezo wa kwenda mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa ambapo kichwa kimoja kilochopokelewa awali kinaendelea kufanyiwa majaribio mbalimbali ya vifaa na kukiendesha na hadi sasa kichwa hiko kimeshapitia majaribio mawili.

“Majaribio hayo ya kiufundi yana awamu ya kwanza inayofanyika kiwandani na awamu zingine kichwa yanafanyika kichwa kitakapofika na sasa tutaenda kwenye majaribio ya kufunga mabehewa na tukijiridhisha ndipo tutaruhusu hatua ya uendeshaji wa kubeba abiria” alisema kaimi Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi Machibya.

Naye Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Ndugu Mrisho Selemani Mrisho ameeleza kuwa TRC inasimamia mradi mkubwa wa kimkakati na bandari inayo furaha kuwa sehemu ya kuhudumia shehena zinazoshusha vifaa vya treni ya umeme ikiwemo vichwa vya treni, mabehewa na reli.

“Sisi kama Bandari tumejipanga vizuri na kazi yetu ni kuhakikisha mzigo unashushwa salama bila ajali yeyote” alisema Bw. Mrisho.

TRC inaendelea kupokea kwa awamu vitendea kazi kwa ajili ya uendeshaji wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR pamoja na kufanya majaribio ya vifaa hivyo ili kujiridhisha kuanza kwa huduma za uendeshaji treni ya umeme mradi wa SGR.