Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

UVCCM WAASA VIJANA NA WATANZANIA KUILINDA RELI YA SGR


news title here
04
July
2024

Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapunduzi Tanzania (UVCCM) wamelitembelea Shirika la Reli Tanzania -TRC kujionea maendeleo ya mradi wa reli ya kiwango cha Kimataifa - SGR Julai 04, 2024.

UVCCM wameitembelea TRC kwa lengo la kujionea ujenzi wa SGR na kuanza kwa shughuli za usafirishaji wa treni za SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambapo walisafiri na treni ya kutoka stesheni ya Dar es Salaam hadi Stesheni ya Pugu.

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndugu Mohammed Ali Kawaida amelipongeza Shirika la Reli Tanzania kwa utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuanza shughuli za uendeshaji wa treni za SGR kutoka Dar es Salaam - Morogoro.

"Sote kama tujuavyo treni ya SGR imeanza safari zake kutoka Dar Es Salaam mpaka Morogoro na mwezi huu Julai 25 tutakwenda kuanza safari za Dar es Es Salaam - Dodoma, hii ni miongoni mwa maagizo waliyopewa TRC na Mheshimiwa Rais kwamba ifikapo Julai TRC wawe wameshaanza safari zao" alisema Ndugu Kawaida.

Aidha, Ndugu Kawaida ametoa wito kwa Vijana na Watanzania wote kuitunza na kuilinda miundombinu ya reli na treni za SGR ili nchi iweze kuendelea na kukua kiuchumi.

"Nitoe wito kwa Vijana wa kitanzania, mradi huu walinzi wake sio Askari polisi peke yao, mradi huu walinzi sio vikosi vya ulinzi pekee yao, mradi huu ulindwe na sisi watanzania wenyewe kwani kusimama kwa mradi wa SGR ni kusimama kwa Maendeleo ya Watanzania" amesema Ndugu Kawaida.

Naye Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa amewapongeza vijana wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania kuitembelea TRC kujifunza teknolojia iliyotumika katika ujenzi na fursa za kiuchumi ambazo zinawafaa Vijana katika kuwanyanyua kiuchumi.

"Haya yote yanafanywa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kwa ajili ya vijana, Sasa vijana mnapoona treni kama hii mnaona nini?, mnaona mazingira mazuri ya kupiga picha (selfie) au mnaona fursa, Serikali kazi yake kubwa ni kutengeneza mazingira ya watu kuweza kufikiri na kutengeneza pesa" amesema Ndugu Kadogosa.

Ikumbukwe kuwa safari za treni za SGR kutoka Dar es Salaam - Morogoro zimeanza Juni 14, 2024 na Julai 25, 2014 Shirika la Reli Tanzania linatarajia kuanza safari za treni za SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.