Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​UTWAAJI WA ARDHI KIPANDE CHA TATU MBIONI KUKAMILIKA


news title here
20
March
2023

Zoezi la uhamishaji makaburi kwaajili ya kutwaa ardhi ambayo inahitajika katika matumizi ya ujenzi wa reli ya kisasa – SGR Mkoani Tabora, kipande cha tatu (3) Makutupora – Tabora linaelekea kukamilika katika Halmashauri ya Tabora, Itigi, Manyoni na Sikonge ambapo ujenzi wa SGR katika kipande hicho umefikia zaidi ya asilimia 5.52% hivi karibuni Machi 18, 2023.

Akizungumza wakati wa kikao cha viongozi na wananchi wa Halmashauri ya Manyoni, Mkuu wa Polisi Manyoni Ahamed Makele – SP ametoa shukrani kwa TRC kwakuanza zoezi la uelimishaji kwa wananchi na viongozi kuhusu zoezi la utwaaji ardhi pia ametoa wito kwa Serikali ya kijiji na ndugu wa marehemu kuendelea kutoa ushirikano wakutosha ili kuhakikisha zoezi linaenda salama.

“TRC mmefanya jambo la msingi sana kuja katika jamii yetu na kuwapa elimu ya uelewa kuhusu utaratibu ambao unatumika katika kuhamisha makaburi, kwa kufanya hivi inasaidia kuondoa migogoro baina ya Serikali na wananchi wake, nitoe wito kwa viongozi na wananchi waendelee kutoa ushirikiano katika zoezi hili na hatimaye kazi iendelee” alisema Mkuu wa Polisi.

Kwa upande wake, Bw. Hassan Simba, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Majengo, Manyoni aliongeza kwa kusema kuwa “Sisi kama viongozi wa maeneo haya tunaahidi kutoa ushirikiano kwa TRC na mkandarasi katika shughuli zote za mradi zinazoendelea katika kata yangu, reli hii ikikamilika itarahisisha shughuli za kijamii na kilimo kwa wakazi wa Manyoni.

Mchungaji Chiristopher Kiwango wa kanisa la Angilikana Itigi, akizungumza kwaniaba ya viongozi wa dini walioshiriki katika zoezi, ametoa shukrani kwa TRC na Serikali ya Wilaya kwa namna zoezi lilivyoendeshwa kwa kuzingatia taratibu za haki na sheria za binadamu, misingi ya imani pamoja na uzingatiaji wa afya wakati wa kuhamisha makaburi.

“Tunaishukru serikali ya Tanzania kwa kutupa viongozi walio simamia zoezi hili kubwa, ambalo limefanyika kwa utaratibu uliozingatia mambo ya afya, imani za marehemu pamoja na haki za binadamu, hivyo tunamshukuru Mungu lakini pia shukrani ziende kwa wale wote walio shiriki katika kazi ya kuhamisha makaburi” Mchungaji alisema.

Aidha, Katika utekelezaji wa ujenzi wa SGR ni ukweli kwamba maeneo mengi ya wananchi yametwaliwa na TRC kwaajili ya kupisha ujenzi wa reli ya kisasa, hata hivyo TRC imekuwa ikitwaa ardhi kwa kuzingatia sheria na kanunu za ardhi ikiwemo malipo ya fidia na Kifuta machozi ambazo ni haki kwa waathirika hao wa mradi.

Mara baada ya kuhamisha makaburi TRC inaendelea na utaratibu wa ulipaji wa kifuta machozi kwa wananchi ambao ni wasimamizi wa makaburi ya ndugu zao yaliyohamishwa kwa lengo la kumpisha mkandarasi kuendelea na ujenzi.