Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​UTWAAJI ARDHI WAENDELEA WILAYANI NZEGA


news title here
28
September
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa- SGR kipande cha nne Tabora - Isaka linalofanyika katika maeneo mbalimbali yaliyopo katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora hivi karibuni Septemba, 2023.

Zoezi hilo linaloambatana na uhamishaji wa makaburi takribani 340 yaliyopo katika vijiji vya Ilole, Luhumbo, Mwino, Kayombo, Malolo, Nawa, Mahene, Bukene na Usongwanhala vilivyopo wilayani Nzega ili kupisha ujenzi wa njia kuu na maeneo ya kuchimba kifusi.

Mthamini kutoka TRC Bi. Tereza Andrew ameeleza kuwa zoezi hilo linafuata taratibu na kanuni zilizowekwa za uhamishaji makaburi katika maeneo pamoja na kushirikisha viongozi husika kuanzia ngazi ya Wilaya hadi wenyeviti wa vijiji husika.

“Kabla ya kuanza zoezi tumewashirikisha viongozi akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Nzega, maafisa afya, maafisa ardhi, watendaji na wenyeviti wa vijiji, viongozi wa dini na kimila pamoja na wananchi” alisema Bi. Tereza.

Aidha, Afisa Afya wa Wilaya ya Nzega Bw. Khalif Salim alisema kuwa zoezi linazingatia usalama wa afya ya wafanyakazi pamoja na wananchi kwa kutumia vikinga ikiwemo barakoa, vikinga mikono, ovaroli na mabuti pamoja na kumwagilia dawa ili kuzuia wadudu wanaoweza kusababisha milipuko ya maradhi kwa njia ya hewa na wale wanaotambaa.

“Tunahakikisha dawa zipo za kutosha na vifaa vya kujikinga wakati wa zoezi zima “ alisema Bw. Khalif.

Mwananchi kutoka katika kijiji cha Ilole , Bwana Amir Hussein ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuleta maendeleo katika maeneo mbali mbali nchini hasa kwenye sekta ya usafirishaji kwa kujenga reli ya kisasa itakayowezesha abiria na mizigo kufika sehemu kwa haraka.

“Tumepata maendeleo kwa kulipwa fidia katika maeneo yetu yaliyo twaliwa na mradi wa SGR na pia vijana wamepata ajira kupitia mradi huu” alieleza Bw. Amir.

Zoezi la utwaaji ardhi ni endelevu linalosimamiwa na TRC pamoja na timu ya maafisa afya na mazingira wa wilaya ya Nzega mkoani Tabora.