ULIPAJI FIDIA WAENDELEA - ZAIDI YA MILIONI 28 ZALIPWA WANANCHI WAFURAHISHWA NA UONGOZI WA RAIS JPM
May
2020
Shirika la Reli Tanzania - TRC laendelea kulipa fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamepitiwa na Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR mkoani Singida Mei 16, 2020.
Zaidi ya Milioni 28 zimelipwa kwa wananchi 101 wa mtaa wa Lusilile kata ya Kitinku Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida ili waweze kupisha mradi wa SGR Morogoro - Makutupora.
Wananchi wa Mtaa wa Lusilile wameshukuru TRC na Serikali kwa ujumla wa kulipa Fidia zao na kuahidi kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu hii hasa katika kuboresha miundombinu.
Bi. Jamila Omary moja kati ya wananchi wa Mtaa wa Lusilile wanaolipwa ameishukuru sana TRC pamoja na Serikali yacawamu ya tano inayoongozwa na Rais Dr.John Pombe Magufuli, kwani wakati wa zoezi hilo linafanyika hakuwa na uhakika kama watalipwa "leo imekuwa kama miujiza kwangu ukizingatia Mtaa huu nilishahama baada ya mume wangu kufariki hivyo mimi ni mjane niliyenufaika namshukuru Mungu kwa jambo hilo“ alisema Bi. Jamila.
Mtendaji wa Kijiji cha Lusilile Bi. Rehema Kahitia pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji hiko Bwana Hussein Kaleso wamewasihi wananchi wa Lusilile kuwa wavumilivu kwa kuwa wote waliopitiwa na Mradi lazima walipwe, kinachotakiwa ni kuendelea kutoa ushirikiano kwa kuleta vielelezo wanavyoagizwa wakati wa utoaji wa Hundi.
Aidha Bwana Seth Exude Afisa Ardhi toka TRC amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwani zoezi hilo lilifanya kwa kuzingatia sheria zote na kama wanaona wanalipwa tofauti na thamani ya Ardhi iliyotwaaliwa Basi waandike barua kwa TRC ili waweze kufanya uthamini tena.
Mthamini kutoka Wizara ya Ardhi Bwana Vincent Ngonyani amesema “kuwa yeyote ambaye wakati uthamini unafanyika hawakuwepo wamuone na ataambatana nao katika maeneo yao kwa ajili ya uthamini na ambaye hakupigwa picha ataandaliwa barua ya utambulisho kutoka kwa Mtendaji hivyo wasiwe na wasiwasi kwani fidia zao lazima zilipwe”.
Shirika la Reli linaendelea kutoa Rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuunga jitihada zinazofanywa na serikali ya Awamu ya Tano katika kuimarisha sekta ya miundombinu ya Reli na ikumbukwe miradi hii imeletwa ili kuleta maendeleo kwa wananchi Watanzania na si kuleta madhara kwa wananchi.