UJENZI WA RELI YA SGR MAKUTOPORA - MWANZA HAKUNA KILICHOSIMAMA
September
2026
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) ikiongozana na Menejimenti imekamilisha ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuanzia Makutopora hadi Mwanza, na kueleza kuridhishwa na hatua kubwa iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR).
Akitathmini matokeo ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRC Bw. Jaffer Machano ameeleza kuwa bodi imekagua maendeleo ya ujenzi kuanzia kipande cha tatu hadi kipande cha tano na kujiridhisha kuwa kazi inakwenda kulingana na mipango iliyowekwa.
Bw. Machano amesisitiza kuwa matarajio ni kukamilika kwa mradi huo na treni ya SGR na kuanza uendeshaji ifikapo mwishoni mwa mwaka 2028 yapo kwenye mwelekeo sahihi na yanasadifu maelekezo ya Serikali.
“Ili kuhakikisha kasi hiyo inadumishwa na kuongezeka, Bodi imetoa maelekezo kwa wakandarasi kuongeza zamu za usiku na kushirikiana kwa karibu na timu ya wahandisi wa TRC waliopo kwenye kila kipande ili kubaini na kutatua changamoto za kiufundi mapema alisema Bw. Machano.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC Mhandisi Machibya Shiwa amebainisha kuwa ujenzi wa Awamu ya Kwanza ya SGR, yenye jumla ya kilomita 1,219 za njia kuu kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza, unaendelea vizuri wakati huduma za treni ya SGR zikiendelea kati ya Dar es Salaam na Dodoma
Pia Mha. Machibya amebainisha kuhusu kujiandaa na msimu wa mvua kubwa nakusema kuwa TRC imeweka mipango madhubuti ya kimkakati ya kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kwenye miundombinu.
“TRC imebainisha kuwa mkakati mkuu utakuwa ni kuhakikisha huduma za usafiri zinarejeshwa kwa muda mfupi zaidi pindi changamoto za mabadiliko ya tabia nchi zinapotokea ili wananchi na wafanyabiashara wasipate usumbufu” alieleza Mha. Machibya.
Mradi huo mkubwa wa SGR unatekelezwa kwa uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sitta chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni hatua ya kuimarisha mfumo wa usafirishaji, kukuza biashara na kufungua fursa za kiuchumi nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Aidha TRC inawasihi wananchi wote kuendelea kulinda na kutunza miundombinu hiyo ya thamani kubwa kwa ustawi wa taifa.

