CAG AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA RELI YA SGR KUELEKEA KIGOMA NA MWANZA
October
2026
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles E. Kichere, amefanya ziara ya siku nne kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR (Standard Gauge Railway) katika vipande vya Makutupora –Tabora, Tabora – Kigoma, Tabora – Isaka na Isaka – Mwanza, kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa miradi hiyo, kubaini changamoto na kuona hatua zinazochukuliwa kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Kichere amesema kuwa kutokana na ukubwa wa uwekezaji katika miradi ya SGR, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ina wajibu wa kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kuleta thamani halisi ya fedha (*value for money*).
“Mradi wa SGR ni mkubwa na unagharimu zaidi ya shilingi trilioni 35. Hivyo, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu ina jukumu la kuutazama mradi huu kuhakikisha fedha za walipa kodi zinatumika ipasavyo na tunapata thamani halisi ya fedha,” amesema Bw. Kichere.
Amesema kuwa kwa ujumla miradi hiyo inaendelea vizuri, huku akilitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuendelea kuwasimamia wakandarasi kwa karibu ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa ubora unaotakiwa na miradi hiyo inatoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Kamishna wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha akimuwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Meshack Anyingisye amesema changamoto chache zilizobainika ziko ndani ya uwezo wa Serikali na wanakwenda kuzifanyia kazi ili kuboresha utekelezaji wa mradi wa SGR.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya M. Shiwa, amemshukuru CAG kwa kutembelea miradi hiyo na kufanya tathmini ya utekelezaji wake. Amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa kwa Shirika na wakandarasi kwa kusaidia kubaini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya TRC, wakandarasi na taasisi za usimamizi wa matumizi ya fedha za umma ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya SGR inatekelezwa kwa kuzingatia ubora, ufanisi na thamani halisi ya fedha zilizowekezwa, ili hatimaye wananchi wanufaike na huduma bora za usafiri wa reli.

