Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC NA ARAB CONTRACTORS ZATIA SAINI MoU, RELI YA MTWARA–SONGEA–MBAMBA BAY


news title here
16
October
2026

Shirika la reli Tanzania (TRC) na kampuni ya Arab contractors ya nchini Misri, zimetia saini hati ya makubaliano kuhusu mradi wa reli ya Mtwara–Songea–Mbamba bay, yenye matawi ya Mchuchuma na liganga, hafla iliyofanyika Oktoba 16, 2026 Jijini Dar EsS alaam, na kushuhudiwa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.

Akizungumza muda mchache baada ya tukio la utaiji Prof. Mbarawa, alisema, mradi wa Reli ya Kusini una umuhimu wa kipekee katika kufungua fursa za kiuchumi katika Ukanda wa Kusini aidha aliongeza kusema kuwa Reli hiyo inatarajiwa kuunganisha Bandari ya Mtwara na maeneo ya uzalishaji wa kilimo, madini na viwanda, hususan miradi ya Mchuchuma na Liganga.

Akitolea ufafanuzi utiwaji Saini huo, Prof. Mbarawa, alisema, ‘’makubaliano yanayosainiwa leo ni hatua ya maandalizi ya mradi huu muhimu.Kupitia ushirikiano huu, tunatarajia kufanyika kwa tafiti za kina zitakazobainisha mahitaji ya usafirishaji, gharama za mradi, manufaa yake ya kiuchumi na njia zinazowezekana za kupata fedha za utekelezaji.

Waziri huyo wa Uchukuzi, Pamoja na mambo mengine, alisisitiza mambo matatu ambayo ni,‘’Kwanza, TRC na Arab Contractors waandae mpango wa kazi wenye majukumu, na matokeo yanayotarajiwa na muda maalumu wa utekelezaji. Pili, tafiti zizingatie uhalisia wa kiuchumi, mahitaji ya mizigo na uwezekano wa kupata fedha za ujenzi na uendeshaji wa reli. Tatu, ushirikiano huu uhakikishe ushirikishwaji wa taasisi muhimu, ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa Tanzania na uzingatiaji wa maslahi ya Taifa’’, alimalizia Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Machibya Shiwa, amesema hati hiyo ya Makubaliano iliyosainiwa inaweka msingi wa ushirikiano katika kufanya tafiti na kuandaa mapendekezo ya kitaalamu na kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mha. Machibya, ameeleza kuwa, kwa mujibu wa makubaliano hayo, Arab Contractors itafanya tafiti za awali na upembuzi yakinifu kwa gharama zake, ikitarajiwa kuwasilisha taarifa ya awali ndani ya miezi mitatu tangu kusainiwa kwa hati hiyo.

”Baada ya kuidhinishwa kwa taarifa ya awali, kampuni itaandaa upembuzi yakinifu wa kina ndani ya miezi tisa, na baadaye kuandaa pendekezo la mradi linalokidhi vigezo vya kupata ufadhili ndani ya kipindi kingine cha miezi tisa” alisema Mha. Machibya.

Aidha Mha. Machibya, alieleza kuwa TRC itatoa ushirikiano wa kitaalamu, kuratibu taasisi na mamlaka zinazohusika, pamoja na kufanya mapitio ya tafiti na mapendekezo yatakayowasilishwa ili kuhakikisha mradi unakidhi mahitaji ya nchi na unatekelezeka kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Mhandisi Machibya, alimalizia kwa kusema kuwa TRC inaendelea kuishukuru Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa mwongozo na usimamizi wake katika maendeleo ya sekta ya reli, huku akieleza matumaini kuwa ushirikiano huo utawezesha Serikali kufanya maamuzi yenye tija kuhusu utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa maendeleo ya Ukanda wa Kusini na Taifa kwa ujumla.