Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

UJENZI WA RELI YA KISASA - SGR WATOA KIPAUMBELE CHA MAFUNZO KWA WAHANDISI WA KIKE 20


news title here
02
October
2019

Shirika la Reli Tanzania nchini - TRC latoa nafasi 20 za mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi miwili katika Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR kwa wahandisi wanawake katika hafla iliyofanyika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya makao makuu TRC Dar es Salaam hivi karibuni Oktoba 01, 2019.

Lengo la kutoa nafasi hizo kwa wahandisi wanawake ni kuwaongezea ujuzi lakini pia kuongeza idadi ya wahandisi wanawake katika Miradi ya Shirika hususani mradi wa SGR ili waweze kujenga na kubuni miundombinu ya reli nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema kuwa Shirika limetoa nafasi hizo ili kuhamasisha wanawake na kuondoa dhana ya kwamba shughuli za uhandisi zinafanywa na wanaume na si wanawake, pia amewaasa kuwa na moyo wa kulitumikia taifa lao na kuwa na uthubutu wa kufanya vitu kwa maendeleo ya taifa.

“Watu wanapopata nafasi ya mafunzo kama haya, ni dhahiri wanapaswa kuyafanyia kazi” alisema Ndugu Kadogosa.

Aidha Ndugu Kadogosa alisema kuwa TRC ni sehemu nzuri ya kupata mafunzo kwa vitendo kwa wahandisi wa nyanja tofauti na pia kuwasihi wahandisi hao kujenga tabia ya kufuatilia miradi ya reli katika nchi za nje kupitia mtandao ili kupata ujuzi zaidi.

Naye Msajili wa Bodi ya Wahandisi kutoka Bodi ya Usajili Wahandisi Tanzania - ERB, Mhandisi Patric Balozi amesema mafunzo haya ya vitendo kwa kundi hili maalumu la wahandisi wanawake yatasaidia kuongeza wingi wa wataalamu hapa nchini na kuacha kutegemea wataalamu wa nje.

“Watanzinia wawe wazalendo kwaajili ya kutumikia nchi yao wenyewe", alisema Mhandisi Balozi

Mhandisi Balozi ametoa shukurani kwa Shirika la Reli Tanzania – TRC kwa kutoa nafasi hii na kusema kuwa wanawake wanapopata nafasi kama hizi wanatakiwa kujituma hali hii itawafanya kuwa wakakamavu na kushirikiana kwa pamoja katika maendeleo ya kujenga taifa.

“Tunawahamasisha wahandisi wa kike ili tusiwapoteze, watumie nafasi hii kujifunza waweze kuwa katika historia ya mradi mkubwa wa SGR" alisema Mhandisi Balozi.

Meneja Mradi ujenzi wa Reli ya SGR kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro Mhandisi Machibya Masanja amesema kuwa kikubwa ni juhudi katika kazi na kujifunza, pia amewakaribisha wahandisi hao kujifunza ili kuweza kuendesha miradi ya reli itakayoendelea nchini.