Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

UFUFUAJI NA UBORESHAJI WA RELI KUTOKA MOSHI – ARUSHA WAFIKIA ZAIDI YA 90%


news title here
20
January
2020

Ufufuaji wa reli yenye umbali wa Kilometa 86 kutoka Moshi – Arusha wafikia zaidi ya 90% tangu kuanza utekelezaji wake ambao utaziwezesha treni za abiria na mizigo zinazoishia Moshi mkoani Kilimanjaro kufika Arusha, hivi karibuni mwezi wa pili 2020.

Lengo la mradi ni kuendelea kuimarisha sekta ya reli nchini kwa kufufuareli ya Kaskazini ili iweze kutoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kwa ufanisi na uhakika kutoka Dar es Salaam, Tanga kuelekea Arusha kama ilivyokuwa zamani zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Kinachoendelea kwa sasa ni kazi ya kubadilisha reli ya zamani yenye uzito wa ratili 45 katika baadhi ya maeneo na kuweka reli yenye uzito wa ratili 60, kutengeneza tuta, kujenga makalavati, madaraja makubwa na madogo na kuimarisha mifumo ya mawasiliano.

Aidha, kazi ya ufufuaji inaendelea kwa kasi ambapo mpaka sasa zimebaki takribani Kilomita 10 kuunganisha njia ya reli kutoka Moshi - Arusha inayotarajiwa kuanza kutoa huduma mapema mwezi Februari 2020.

Mradi huu umetoa fursa ya ajira kwa wananchi wa Kaskaziniambapo watu zaidi 561 wameajiriwa wakiwemo wasimamizi, mafundi 125 na vibarua 358. Reli hii itakapoanza kutoa huduma itawasaidia wananchi wa Arusha kuendesha shughuli za kijamii, biashara na uchumi kwa haraka na kusaidia kuinua uchumi wa taifa kupitia usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya reli.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Ufufuaji reli Moshi - Arusha Mhandisi Shadrack Masawe, ameeleza jinsi kazi ya ufufuaji reli na ujenzi wa miundombinu wezeshi inavyoendelea “tunaondoa reli ya zamani yenye uzito wa ratili 45 na kuweka reli yenye uzito wa ratili 60 ili kuongeza mwendokasi na ufanisi katika ubebaji mizigo. Kipande hiki cha reli ya Moshi - Arusha kilikuwa kimeharibika sana, asilimia 85 ya tuta ilikuwa imechukuliwa na maji, madaraja mengi yalikuwa yamevunjika lakini pia ya reli 1300, mataruma 1400 na vifungashio 50,000 viliibiwa” alisema Mhandisi Masawe.

Mhandisi Masawe ameongeza kuwa “Kazi tunayofanya sasa ni kuhakikisha miundombinu hii tunairudishia na kuiboresha, tayari kuanza kutoa huduma kwa ufanisi”.

Naye Bi. Farida Msemo ambaye ni mnufaika wa mradi huu amesema kuwa “kilichonisukuma sana ni changamoto za ajira, baada ya Rais Magufuli kutangaza mradi huu kwanza nilipata mwamko wa kushiriki kufanya kazi, binafsi tunaishukuru Serikali kupitia Shirika la reli kwa kutupa ajira bila kujali jinsia, mradi huu umetupatia ujuzi mwingi lakini pia tunapata kipato cha kuendesha familia zetu”.