Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TUKO TAYARI KULINDA MIUNDOMBINU YA RELI YA SGR: WANANCHI KILOSA


news title here
05
November
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la utwaaji ardhi kupisha mradi wa ujenzi wa reli yenye kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha pili Morogoro - Makutupora lililofanyika wilayani Mvomero pamoja na wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro hivi karibuni Novemba 2023.

Zoezi linaambatana na uhamishaji makaburi yaliyopo katika kijiji cha Kimambila wilayani Mvomero na kijiji cha Mwasa kilichopo katika wilaya ya kilosa kwa lengo la kupisha njia za vivuko.

Mhandisi kutoka TRC Bw. Juma Kadashi alisema kuwa wananchi wametoa ushirikiano mzuri katika kuhakikisha zoezi la utwaaji ardhi linafanyika kwa kufuata taratibu na kuahidi kulinda miundombinu ya reli ya SGR.

“Zoezi linaendelea vizuri, tumeshirikisha wananchi pamoja na viongozi wa kijiji pia zoezi linasimamiwa na maafisa afya kwa kufuata taratibu zote za kiafya kuepusha magonjwa ya milipuko” alisema Mhandisi Kadashi.

Mwenyekiti kutoka katika kijiji cha Mwasa Bw. Juma Hamadi ameeleza kuwa kupitia mradi wa SGR wanakijiji wamepata manufaa makubwa ya kimaendeleo ikiwemo kuboresha makazi, biashara na kilimo na pia vijana wengi kujipatia kipato kwa kupata ajira ndani ya mradi huo wa SGR.

“Wananchi wako tayari kuilinda miundombinu ya reli ya SGR na watakuwa na nguvu kubwa endapo wataachiwa barabara ya mradi itumike pia katika matumizi ya wanakijiji kwani ina msaada mkubwa kwao” alisema Bw. Juma.

Naye Mwananchi wa kijiji cha Mwasa Bw. Richard Kitali alisema kuwa mradi umeleta manufaa kwa vijana, kina mama na wana kijiji kwa ujumla na kupitia reli ya SGR usafiri utakua na urahisi na vijiji kukua kibiashara na kiuchumi.

“Hii reli ni yetu na tuko tayari kuilinda kwa hali na mali kwa manufaa yetu sote na taifa letu“ alisema Bw. Kitali.

Zoezi la utwaaji ardhi kupisha mradi wa SGR katika maeneo ya vivuko na njia ya umeme unaendelea hadi mkoani Dodoma.