TRENI YA KWANZA YA MIZIGO YAWASILI KATIKA BANDARI KAVU YA KWALA.

May
2020
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye amezindua rasmi bandari kavu ya Kwala ambapo Treni ya Kwanza iliyobeba Behewa za mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam imewasili katika Bandari hiyo iliyopo Kibaha mkoani Pwani hivi karibuni Mei, 2020.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Mkuu mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Everist Ndikilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka wa Bandari Tanzania Mhandisi Deusdedith Kakoko, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa na wafanyakazi kutoka taasisi tajwa.
Bandari iliyozinduliwa ina umuhimu mkubwa, kwani itasaidia kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam, itaweza kusaidia utunzaji wa barabara ya Morogoro kwa kuwa bila bandari ya Kwala mizigo ingekuwa ingepaswa kusafirishwa na Malori ambayo yangeharibu barabara ya Morogoro. Kufuatia hatua hiyo hivi sasa wafanyabiashara watakuwa wanachukua mizigo yao katika bandari hii.
‘’Niwahakikishie Watanzania na wadau wote wa Mamlaka wa Bandari Tanzania kuwa mizigo haitarundikana katika Bandari ya Dar es salaam lakini pia huku inakoletwa haitarundikana, tunategemea wadau mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania - TRA na wengine waje kufanya ‘logistics’ za kutoa mzigo kwa haraka na kuondoshwa kwa haraka na tunategemea kutakuwa na maegesho mengi sana hivyo malori mengi yataingia na kushusha mizigo kwa haraka” alisema Mhandisi Nditiye.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo amesema muingiliano wa watu na mali utakuwa mkubwa katika bandari hiyo, hivyo moja kati ya mambo ya kufanya kama Mkuu wa Mkoa ni kuhakikisha mali za wananchi zinakuwa salama na vyombo vya dola vinafanya kazi kikamilifu ikiwepo polisi, najua kuna RPC wa Bandari lakini inabidi ashirikiane na RPC wa Mkoa wa Pwani.
Halikadhalika Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Mhandisi Deusdedit Kakoko amesema kuwa mamlaka ya Bandari, wajumbe wa bodi tukiwa na mwenyekiti wa bodi tutahakikisha tunamaliza kazi kwa muda uliopangwa na kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali kupitia Wizara hili eneo lazima lianze kufanya kazi rasmi mwezi wa saba lakini tutaendelea kuleta makasha kuhakikisha yanapatikana pindi tunapoanza biashara.
Aidha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kungu Kadogosa amesema shirika lipo tayari na lina uwezo wa kuingiza treni za Behewa 20 na makasha yake, pia tunaweza kuleta treni tano zenye Behewa 20 kila moja, hata hivyo tunaweza kuongeza zaidi kwa kuwa tunajenga wenyewe na pindi reli ya kisasa itakapoanza itafanya kazi kwenye bandari hii.
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Huduma toka Shirika la Reli Tanzania Ndugu Focus Makaye Sahani amesema Shirika limejipanga vizuri kwani linategemea vichwa toka Morogoro kwa kazi hii na tayari Behewa 44 mpya zipo kwa ajili ya kazi hiyo, hivyo kazi itafanyika kwa urahisi.