TRENI YA DELUXE ILIYOBEBA WASANII WA WCB YAWASILI KIGOMA NA KUPOKELEWA NA MAMIA YA WANANCHI
December
2019
Treni ya Kisasa ya Deluxe ya Shirika la Reli Tanzania - TRC iliyobeba wasanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka kampuni ya Wasafi Classic Baby (WCB) imewasili mkoani Kigoma ikitokea Dar es Salaam hivi karibuni Desemba 2019.
TRC kwa kushirikiana na kampuni ya WCB hivi karibuni waliandaa safari kuelekea Kigoma kwa kutumia treni ya kisasa ya Deluxe kwa lengo la kuhamasisha watanzania kutumia usafiri wa treni, kutangaza huduma ya Miradi ya Shirika pamoja na kuhamasisha watanzania kulinda miundombinu ya reli.
Katika safari hiyo iliyohusisha wasanii zaidi ya 200 wa muziki wa kizazi kipya kutoka kampuni ya WCB na wasanii wengine wa muziki wa kizazi kipya ilikuwa pia na lengo la kuadhimisha miaka 10 ya Msanii ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya WCB Diamond Platnum katika tasnia ya muziki nchini.
Kama ambavyo abiria wengine wamekuwa wakipata fursa ya kufurahia safari ambayo huwa zaidi ya safari kwa kutumia treni, wasanii nao walipata fursa ya kuona mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR unaotekelezwa kuanzia Dar es Salaam hadi Makutupora Singida kwa fedha za watanzania wazalendo ambapo pia walitembelea handaki namba mbili ambalo ni refu zaidi nchini lenye urefu wa KM 1.031 kwa ajili ya kupitisha reli ya SGR Kilosa mkoani Morogoro.
Aidha wasanii hao wameonekana kufurahishwa na huduma za treni ya kisasa ya Deluxetangu mwanzo hadi mwisho wa safari kutokana na huduma nzuri pamoja na burudani zinazopatikana ndani ya treni hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kadogosa amesema kuwa wasanii hao wameonesha uzalenda wa aina yake kwa kujali vya kwetu, kwani wametoa muda wao na fedha zao kutumia usafiri wa treni kwa lengo la kuutangaza usafiri huu pamoja na Shirika kwa ujumla, kwa kipekee ametoa shukurani kwa wasanii na kampuni ya WCB kwa uzalendo wao.
Nasib Abdul maarufu kama Diamond Platnum kwa niaba ya Kampuni ya WCB amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa TRC kwa utayari aliouonesha tangu siku ambayo walipeleka maombi ya safari hiyo na ushirikiano uliokuwepo katika safari kuanzia Dar es Salaam hadi Kigoma.