Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRENI ILIYOBEBA MASHABIKI WA SIMBA NA YANGA YAANZA SAFARI KUELEKEA KIGOMA


news title here
23
July
2021

Treni ya Deluxe iliyobeba Wasanii na Mashabiki wa mpira wa miguu imeanza safari katika Stesheni ya Kamata jijini Dar es Salaam kuelekea Kigoma kwenye mechi kati ya Simba na Yanga inayotarajiwa kuchezwa Julai 25, 2021.

Shirika la Reli kwa kushirikiana na Clouds Media Group wameandaa safari hiyo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza sekta ya michezo na burudani lakini pia kutoa fursa kwa wananchi kutumia huduma ya usafiri reli ambao kwa sasa umeboreshwa zaidi.

Treni hiyo imeondoka katika Stesheni ya Kamata jijini Dar es Salaam Ijumaa na inatarajiwa kufika Kigoma mapema siku ya Jumamosi ambapo pamoja na mambo mengine treni hiyo ina huduma zote muhimu ikiwemo chakula, vinywaji pamoja na burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wa Bongo Fleva akiwemo Juma Nature, Chege, Lulu Diva, Sholo Mwamba, G Nako na Lina.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameeleza kuwa safari hiyo ni zaidi ya safari lakini pia amesisitiza kuwa tahadhari za kiafya dhidi ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona zinazingatiwa katika safari hiyo ambapo pamoja na hatua nyingine idadi ya Behewa za treni hiyo ni 14 zitakazowezesha kupunguza msongamano kwa kiasi kikubwa kulingana na idadi ya abiria wanaosafiri.

“Tutasafiri pamoja na nina imani safari yetu itakuwa ya kitalii, mtapatafursa ya kuona maendeleo ya mradi wa SGR pamoja na kuona Mahandaki ya reli” alisema Kadogosa

Msanii wa Bongo Fleva Saidi maarufu Chege ameeleza kuwa yeye ni miongoni mwa wasanii waliomo katika msafara huo ambapo wanakwenda Kigoma kwenye tamasha pamoja na wasanii wengine lakini pia kuona mchezo wa mpira wa miguu utakaochezwa kati ya Simba na Yanga siku ya Jumapili Julai 25, 2021.

Bakari Juma ni Shabiki wa mpira wa miguu ameeleza kuwa usafiri wa reli ni salama kuna burudani, vinywaji na burudani nyingine ambazo zinamfanya abiria asichoke kusafiri.

Shirika la Reli limekuwa likishirikiana na taasisi na mashirika ya umma na binafsi kutooa huduma ya usafiri kwa makundi maalumu katika matukio tofauti kwa lengo la kutoa huduma na kuunga mkono jitihada za serikali kuleta maendeleo katika nyanja zote.