Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YATWAA ARDHI SHINYANGA MANISPAA KUENDELEZA UJENZI WA SGR KIPANDE CHA TANO ISAKA - MWANZA


news title here
15
September
2022

Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea kutwaa ardhi katika manispaa ya Shinyanga kupisha mradi wa reli ya kisasa katika kipande cha Tano ambacho ni Isaka - Mwanza, Septemba 2022.

Ardhi hiyo imeongezwa kupitia zoezi la uhamishaji makaburi lililosimamiwa na Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga kwa lengo la kukabidhi ardhi kwa mkandarasi wa ujenzi wa reli ya kisasa Mwanza - Isaka.

TRC imetwaa ardhi katika vijiji vya Mwalugoye, Mwamalili, Mwamala, Negezi, Azimio, Lubaga, Ihapa na Old Shinyanga pamoja na Isaka kwa lengo la kumpatia eneo mkandarasi wa mradi wa SGR kipande cha tano Isaka - Mwanza.

Afisa Ardhi na Miliki kutoka TRC Paschal Thomas Sinyaw amesema zoezi limekwenda vizuri na wananchi wametoa ushirikiano kupitia elimu waliyopewa na watalaamu wa ardhi kutoka Halmashauri husika kuhusu uhamishaji wa makaburi kwa ajili ya kupisha eneo hilo kutumika kujenga miundombinu ya SGR katika maeneo hayo.

“Zoezi la kuhamisha makaburi linafanywa na watalaamu kutoka halmashauri au manispaa husika ambapo tuna watalaam ambao ni afisa ardhi na maafisa wa afya kutoka Manispaa ya Shinyanga, Afisa Ardhi na Maafisa wa afya kutoka Halmashauri ya Msalala kwahiyo sisi TRC tupo hapa kwa ajili ya kuhakikisha maeneo yanayohamishwa makaburi ni sahihi kulingana na taarifa zilizowasilishwa vilevile zoezi limehusisha viongozi wa vijiji, wananchi pamoja na viongozi wa Dini "ameongeza Paschal.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Isaka Shabaan Jumanne Hamisi amewapongeza wananchi waliotwaliwa maeneo kwa kutoa ushirikiano kwa TRC na Serikali kwa kukubali kuhamisha makaburi ili kupisha ujenzi wa mradi wa reli unaopita kijijini hapo.

"Wananchi wameelewa umuhimu wa huu mradi na pia wanafahamu kama ni mradi chanya kwa watanzania, vilevile tumehamasika kwa miji inayokua hatutakiwi kuzikia majumbani bali tutenge eneo ambalo litakua maalumu kwaajili ya mazishi ili kuepusha uhamishaji wa makaburi endapo patatokea tena mradi mwingine wa kimaendeleo kama huu wa SGR" alisema Shabaan Jumanne.

Naye Mkazi wa Mwalugoye Isack Ndila Makoye ameipongeza TRC kwa kuweza kufanya uthamini wa ardhi wa haki pamoja na elimu iliyotolewa kwa wananchi wote waliotwaliwa maeneo yao kijijini hapo na amefarijika kua mmojawapo kushiriki kwa namna ya kipekee katika ujenzi wa Reli ya Kisasa.

“Najisikia Fahari kua sehemu ya mradi maana kutoa ardhi ni kushiriki katika maendeleo ya nchi na huu mradi utaturahisishia mambo mengi ikiwemo kusafiri kwa muda mfupi na pia kusafirisha bidhaa zetu kwa haraka zaidi na hii itaamsha watu wengi kufanya biashara kwa sababu usafiri utakua wa uhakika kutoka Dar hadi Mwanza” ameongeza Isack Makoye.

Hiki ni kipande cha Tano cha mradi wa SGR kinachosimamiwa na Shirika la Reli Tanzania ambacho ni Isaka - Mwanza na kipande hiki kimefikia asilimia 12.3 za ujenzi toka kilivyoanza .