Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YATOA MAFUNZO KWA WANANCHI JUU YA KUJIKWAMUA KIUCHUMI


news title here
19
February
2021

Shirika la Reli Tanzania - TRC limetoa mafunzo kwa wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa na mradi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro kuhusu njia mbalimbali za kujikwamua kiuchumi, yaliyofanyika katika ofisi ya kata ya Pugu, eneo la Pugu Stesheni pamoja na halmashauri ya wilaya ya Kisarawe hivi karibuni Februari 2021.

Mafunzo hayo ambayo yamegawanyika katika makundi tofauti ujasiriamali, ufundi stadi, kilimo cha kisasa na ufugaji pamoja na urasimishaji wa ardhi na hati miliki ambapo yatawasaidia wananchi waliopatiwa malipo yao ya fidia kwa kiasi kikubwa katika kujikwamua kiuchumi.

Afisa wa masuala ya jamii kutoka TRC Bi. Lightness Mngulu ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutoa mwanga na kuwawezesha wananchi wote waliotwaliwa maeneo kupisha mradi wa SGR kujifunza na kupata elimu ya mambo mbalimbali ya kujiinua kiuchumi.

Bi. Lightness amesema kuwa mafunzo hayo yametolewa na wajuzi mbalimbali wakiwemo afisa kilimo na mifugo, afisa ardhi, wajuzi wa ufundi stadi na wajasiriamali kutoka katika maeneo tofauti ya kata ya Pugu pamoja na Wilaya ya Kisarawe.

”Tumewashirikisha watu wenye ujuzi katika nyanja tofauti ili wawe wakufunzi na wananchi waweze kuwapata kwa urahisi” alisema Bi. Lightness.

Vilevile Bi. Lightness amewaasa wananchi kuweka umakini katika kile wanachojifunza na kujitokeza kwa wingi kupata mafunzo hayo ambayo ni muendelezo ambapo mafunzo hayo hayana gharama yeyote kwa mwananchi.

“Mafunzo haya ni burena yanafaida kubwa kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi” aliongezea Bi. Lightness.

Nae mkazi wa eneo la Pugu Stesheni Bi. Pili Salumu ametoa shukrani kwa serikali ya awamu ya tano pamoja na TRC kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia wananchi wengi kujiendeleza na kujiinua kiuchumi.

“Mafunzo ni mazuri sana na yanasaidia mwananchi kutunza pesa na kuwa na umakini na ustadi” alisema Bi. Pili.

Naye fundi chuma katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Bw. Alila Bakari amesema kuwa wamefurahishwa sana na ujio huo wa TRC wilayani humo na kutoa mafunzo kwa wananchi ambayo yatasaidia hadi vizazi vya baadae na vya sasa kuweza kujikwamua kiuchumi na maendeleo.

“Mafunzo haya yana tija kwakua mtu akipata elimu na ujuzi basi atafundisha wengine katika jamii” alisema Bw. Alila.