Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YASISITIZA KUWEPO KWA MPANGO WA USIMAMIZI WA WAFANYAKAZI KATIKA MRADI WA SGR


news title here
08
June
2025

Maafisa kutoka Idara ya Rasilimali watu na Utawala, Kitengo cha Jamii na Kitengo cha Habari na Uhusiano cha Shirika la Reli Tanzania (TRC), Juni 07, 2025 wameendelea na zoezi la kampeni ya elimu na Uhamasishaji kuhusu Mpango na Taratibu za Usimamizi wa Wafanyakazi (LMP - Labour Management Producer) katika mradi wa SGR.

Zoezi hilo limewafikia wakandarasi na wafanyakazi wanaotoa huduma za ulinzi na usafi ndani ya treni na stesheni zote ikiwemo SumaJKT, Service Hub, Jofort Intertrade co. Ltd na kampuni tanzu ya TRC TANRAIL.

Elimu hili inatolewa katika stesheni zote za SGR na mpaka sasa elimu imewafikia watoa huduma wa usafi na ulinzi katika stesheni ya Magufuli, Pugu, Soga, Ruvu, Ngerengere, Morogoro, Mkata, Kilosa, Kidete,Gulwe, Igandu na Samia Stesheni. Zoezi hili ni endelevu katika kuhakikisha uendeshaji salama wa mradi wa SGR.

Afisa Tawala Mkuu kutoka TRC Bi. Miriam Kasanga, amesema kuwa lengo la kampeni hii ni kutoa elimu na uhamasishaji kwa usimamizi wa wakandarasi na wafanyakazi katika uendeshaji kwa kuzingatia haki za wafanyakazi, Afya na usalama kazini (OHS), kuzuia ukatili wa kijinsia (GBV), unyonyaji na udhalilishaji wa kingono (SEA), unyanyasaji wa kijinsia (SH), pamoja na kuundwa kwa mfumo na taratibu za kushughulikia malalamiko ya wafanyakazi na wateja (GRM).

"Tukumbuke tu tukisema taratibu za usimamizi wa kazi tunamaanisha mikataba ya ajira, likizo, taratibu za kuacha kazi au kuachishwa kazi, masaa ya kazi, matumizi ya vifaa kinga na utoaji wa elimu kwa wafanyakazi kuhusu haki zao za msingi" amesisitiza Bi. Miriam Kasanga.

Katoka hatua nyingine, Oscar Juma Rashid mfanyakazi wa Service Hub ameishukuru TRC kwa kutoa elimu hii kwani imemsaidia kufahamu haki zake za utaratibu wa ajira ikiwemo umuhimu wa kuwa na mkataba kazini, haki ya likizo na kupata mshahara kwa wakati.

Shirika la Reli Tanzania - TRC lina jukumu la kuhakikisha kua wakandarasi wake wanasimamia na kutekeleza kikamilifu masharti yote yanayohusiana na haki na ustawi wa wafanyakazi kwa kufanya ukaguzi na ufuatiliaji endelevu katika kuhakikisha kua wakandarasi wanatekeleza kikamilifu mahitaji ya Mpango wa Usimamizi wa wafanyakazi (Labour Management Plan - LMP).