Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YASHIRIKISHA KAMATI ZA ULINZI NA USALAMA ZA WILAYA KUWA MABALOZI WA ULINZI NA USALAMA WA RELI


news title here
10
May
2024

Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea na zoezi la kuhamasisha, kuelimisha na kushirikisha viongozi wa ngazi mbalimbali kufuatia zoezi la uwekaji mageti kwenye njia ya mradi wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR kipande cha pili cha Morogoro - Makutupora hivi karibuni, Mei 2024.

Lengo la kampeni ya uhamasishaji na uelimishaji viongozi ni kuongeza hamasa katika kuilinda miundombinu ya reli, kuhamasisha usalama wa wananchi na mali zao na kupokea maoni na mapendekezo ya viongozi juu ya umuhimu wa uwekwaji wa mageti na uzio katika njia ya reli ya SGR.

Kampeni inafanyika katika ngazi mbalimbali za jamii ikishirikisha Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa Wilaya, Viongozi wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji, Madiwani, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa vyama vya Siasa pamoja na wazee maarufu wa Vijiji na Mitaa.

Mratibu Msaidizi Mazingira na Jamii kutoka Shirika la Reli Tanzania Bi. Glory Mrengo ameeleza kuwa TRC imeendelea kushirikiana na viongozi mbalimbali katika kuhakikisha wananchi wanaelewa vyema umuhimu wa ujenzi wa SGR pamoja na masuala ya kuzingatia katika kuhakikisha usalama na ulinzi wa miundombinu ya reli.

"Ni wajibu wa kila kiongozi kuwaelimisha wananchi waelewe vyema umuhimu wa ujenzi wa SGR, waelewe kuwa SGR ni mali yao hivyo wana wajibu wa kuitunza ili kuleta maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla" Amesema Bi. Mrengo.

Aidha, Bi.Glory ameongeza kuwa kuelekea kuanza shughuli za uendeshaji wa treni za SGR Shirika la Reli Tanzania limejikita kuhakikisha Sheria, Kanuni na Taratibu zinazostawisha maendeleo ya jamii zinatekelezwa ikiwemo ujenzi wa fensi na uwekaji mageti kwaajili ya usalama wa raia.

"Shirika la Reli Tanzania linaongozwa na Sheria, Kanuni kanuni, Taratibu za ustawi wa jamii na maendeleo za Kitaifa na Kimataifa hivyo kuwashirikisha viongozi ni takwa la kisheria katika kuilinda miundombinu ya reli pamoja na watu ili kuepusha ajali na kulinda Mazingira, kwahiyo mageti haya yatawekwa kwa ajili ya Ulinzi na Usalama" Amesema Bi. Glory.

Afisa Mtendaji Kata ya Zuzu Bwana Jafet Richard amesema kuwa kupitia elimu na uhamasishaji wanayopewa viongozi imewafanya kuwaelimisha wananchi kuhusu mradi wa SGR katika masuala mbalimbali ikiwemo Ulinzi na Usalama pamoja na upatikanaji wa WA fursa mbalimbali za kiuchumi.

"Mimi nimeona ili mnalofanya TRC ni jambo zuri sana, elimu hizi zimetuwezesha sisi viongozi kuelewa vizuri huu mradi, tumekuwa mabalozi wazuri katika kuwapa ujuzi wananchi wetu , mimi nimewaandaa wananchi wangu kuona fursa ya kuuza mboga mboga zinazolimwa kuzunguka bwawa la Pinda , treni ikianza wataweza kufikia masoko makubwa kama Dar es Salaam na mengine" Amesema Bwana Jafet.

Kuelekea kuanza kwa shughuli za uendeshaji treni za SGR Shirika la Reli Tanzania limejikita katika kuhamasisha wananchi kuendelea kuzingatia masuala ya usalama ili kuilinda miundombinu ya Reli pamoja na kuokoa maisha na mali za wananchi.