TRC YASHIRIKI MAONESHO YA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA MUUNGANO
April
2024
Shirika la Reli Tanzania - TRC limeshiriki maonesho ya Muungano katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania yaliyofunguliwa na Makamu wa pili wa Rais Zanzibar Mhe. Ahmed Suleimani katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Aprili 2024.
Meneja Msaidizi wa kipande cha kwanza Mhandisi David Msusa amesema kuelekea miaka 60 ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania TRC imeweza kusimamia ujenzi wa mradi wa kimkakati wa ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa - SGR ambao unatekelezwa na Serikali ya awamu ya sita kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na Tabora hadi Kigoma.
"Kuelekea miaka 60 ya Muungano TRC inatarajia kuanza safari za treni za abiria mwezi Julai kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na maandalizi yamefanyika ya kutosha na vitendea kazi vimewasili na timu ya wataalamu inaendelea na majaribio ya safari za treni ya abiria kutoka Dar es salaam hadi Dodoma" ameongeza Msusa.
Pia Mhandisi Msusa ameongeza kuwa reli ya SGR inatumia mwendokasi wa kilomita 160 kwa saa na treni ya mizigo itakua na uwezo wa kubeba takribani tani elfu kumi kwa safari.
TRC inasimamia uendeshaji wa reli ya kati (MGR) na reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) pamoja na miradi yote inayoendeshwa TRC ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya reli.