TRC YASHIRIKI BONANZA LA MICHEZO PAMOJA NA SEKTA NYINGINE ZA UCHUKUZI

March
2020
Shirika la Reli Tanzania - TRC lashiriki Bonanza la michezo la taasisi za Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Sekta ya uchukuzi lililofanyika katika uwanja wa TCC Club Chang’ombe jijini Dar es Salaam Machi 7, 2020.
Lengo la Bonanza hilo ni kuimarisha afya na utendaji wa watumishi walio chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano hususani sekta ya uchukuzi pia limelenga kuimarisha umoja na kubadilishana mawazo kati ya watumishi wa taasisi za uchukuzi nchini
Bonanza hilo lililoandaliwa na Shirika la Reli nchini limeshirikisha taasisi za serikali ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania – TPA, Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege – TCAA, Mamlaka ya Usafiri wa Anga - TAA, Kampuni ya Ndege Tanzania – ATCL, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania – TMA, na ‘Tanzania International Container Terminal Services’ (TICTS) ambapo mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho alifungua rasmi bonanza hilo.
Aidha, michezo ambayo imechezwa katika Bonanza hilo ni pamoja na mpira wa miguu, karata, molpira wa watu, drafti, kuvuta kamba, mbio za magunia, bao na kukimbiza kuku ambapo timu ya mpira wa miguu kutoka TICTS iliibuka kidedea dhidi ya timu ya TRC katika mchezo huo na kupata kikombe ikifuatiwa na timu ya TRC ambayo ilipata nafasi ya pili na kuzawadiwa kikombe, halikadhalika washindi wengine waliopata zawadi ni pamoja na mshindi wa kwanza katika mchezo wa mpira wa wavu ambaye ni timu ya Uchukuzi na mshindi wa pili wa mchezo huo amabaye ni timu ya Shirika la Reli.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Bonanza hilo Katibu Mkuu Wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Leonard Chamuriho amewapongeza watumishi waliojitokeza kwa katika bonanza hilo na kusema kuwa afya ikiwa nzuri hata utendaji kazi unakuwa mzuri hivyo amewasihi watumishi kushiriki michezo mara kwa mara ili kuimarisha afya, pia amelipongeza shirika kwa maandalizi mazuri ya bonanza hilo.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kadogosa amewashukuru washiriki wote walioshiriki na amesema kuwa Shirika litaendelea kuhakikisha linaandaa mabonanza mengine mengi pamoja na kuendelea na utaratibu wa kufanya mazoezi jumamosi moja ya kila mwezi ili kuhakikisha afya za watumishi zinakuwa nzuri. Pia amemshukuru Dkt. Chamuriho kwa kujumuika pamoja katika bonanza hilo.