Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YAPOKEA VICHWA VIPYA VITATU VYA TRENI ZA RELI YA MGR


news title here
17
November
2021

Shirika la Reli Tanzania – TRC limepokea vichwa vitatu vya treni za reli ya MGR, vichwa hivyo vimenunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Reli ya Kati - TIRP, hafla fupi ya upokeaji imefanyika katika bandari ya Dar es Salaam Novemba 17, 2021.

Serikali imenunua vichwa hivyo kutoka Kampuni ya SMH RAIL ya nchini Malaysia na kuvisafirisha kwa njia ya meli iliyowasili bandari ya Dar es Salaam tarehe 15 Novemba 2021. Lengo la manunuzi ya vichwa hivyo ni kuvuta behewa za mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi bandari Kavu ya Isaka (970km).

Pamoja na hivyo, Shirika la Reli ya Tanzania linaendelea na uboreshaji wa huduma ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli kutoka Dar es Salaam hadi Bandari Kavu ya Isaka (970 km). Mradi huo unatekelezwa kwa kutumia fedha ya mkopo wa Dola za Marekani milioni 300 kutoka Benki ya Dunia.

Sambamba ya ujio wa vichwa vipya vya treni, Shirika la Reli nchini limefanikiwa kwa 80% katika usafirishaji wa mzigo ambapo mwaka 2020/2021 liliweza kubeba tani za mizigo 320,106 ambapo lengo lilikuwa ni tani 400,000 kwa mwaka, hivyo Shirika lina matumaini na uhakika wa kusafirisha tani nyingi za mizigo kwa mwaka fedha 2021/2022 kutokana na ujio wa vichwa hivi vitatu vipya ambavyo vitaongeza kasi ya ubebaji mizigo kutoka katika bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ambaye ni Mgeni Rasmi amesema kuwa mahitaji ya behewa na vichwa vya treni kwa ajili ya kuhudumia wateja wa nje na ndani ya nchi kwa sasa ni mkubwa. Kutokana na hali hiyo imepelekea Serikali kuboresha zaidi sekta ya reli hii ili kuendelea kutoa huduma bora, salama na uhakika kwa wadau kwa kununua vichwa vipya vitatu 3.

Aidha, Mhe. Waziri alisisitiza kuwa mara baada ya Serikali kununua vichwa vipya vitatu vitaongeza ufanisi mara mbili pamoja pato kwa Shirika kutokana na uwezo wake mkubwa ukilinganisha na vinavyotumika kwa sasa. ”Ujio wa vichwa hivi ni ukuzaji wa uchumi, vitakuwa na uwezo mkubwa wa kuvuta mzigo mkubwa, ambapo shirika litakuwa na uwezo wa kusafirisha tani 7,000 mpaka 10,000 za mizigo kwa mwezi, na kuliingizia Shirika kiasi cha Dola za Marekani 3,503,990 kwa mwaka” alisema Prof. Mbarawa.

Mhe. Waziri wakati akipokea vichwa hivyo alipata wasaa wa kutoa angalizo kwa watendaji wote wataoviendesha vichwa hivyo kuwa waadilifu na wazalendo.

“Angalizo langu ni kwamba vichwa hivi tumevinunua kwa gharama kubwa dola za Marekani milioni 9.1, kwa wale watakaopata dhamana ya kuendesha wawe waadilifu, wazalendo na wafanye kazi kwa ufanisi, hatutegemei kusikia vichwa hivi tulivyonunua kwa gharama kubwa vinaanguka” alisema Prof. Mbalawa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Shirika la Reli Tanzania amesema kuwa mahitaji yamekuwa makubwa na nchi inazidi kupanuka, watu wananongezeka na shughuli za uchumi nazo zinazidi kuongezeka sambamba na uzalishaji wa mali, kutokana na mahitaji kuongezeka reli inahitajika pamoja na vichwa hivi vitatu navyo ni sehemu ya uwezeshaji wa ufanisi wa reli ya kati.

Prof. Kondoro aliongeza kuwa “kama tunavyoona mahitaji ya hapa nchini yameongezeka hata mahitaji ya nchi jirani yanazidi kuongezeka, kwa namna jografia ya nchi yetu ilivyokaa ni rahisi katika muingiliano wa nchi nyingine hivyo reli yetu ni muhimu sana”.

Naye Mkurugenzi Mkuu TRC alizungumzia kuhusu uwezo, ufanisi na ubora wa vichwa hivyo.

“Vichwa hivi vina uwezo mkubwa ambapo kichwa kimoja kina nguvu ya ‘Horse Power 3000’ na kina uwezo wa kuvuta behewa 20 sawa na tani 1200 kutoka Dar es salaam hadi Morogoro tofauti na awali ambapo vilikuwa vikifungwa vichwa viwili kwa sababu ya mwinuko mkali uliopo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro. Kuanzia Morogoro kichwa kimoja kitaongezewa mzigo hadi kufikia tani 2000 ambazo ni sawa na behewa 33” alisema Mkurugeza TRC.

Pia Kadogosa aliongezea kuwa, usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli utapunguza uharibifu wa barabara kwa kiasi kikubwa, vilevile vichwa hivi vipya vimefungwa kifaa chenye uwezo wa kutoa taarifa kwa waongoza treni kwa njia ya mtandao ili waweze kufuatilia mwenendo wa treni kuanzia Dar es Salaam hadi mwisho wa safari. Taarifa zitakazopatikana ni mwendokasi wa treni, aina ya treni, matumizi ya mafuta, mahali treni ilipo na hitilafu ya kichwa cha treni ili kupata ufumbuzi wa haraka. Taarifa hizi zitaongeza ufanisi na kuimarisha usalama wa safari ya treni.