Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAPOKEA MAKASHA YA UBARIDI KUTOKA WFP


news title here
11
September
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limepokea makasha matano ya ubaridi kwaajili ya kusafirisha matunda na mbogamboga kwa kutumia usafiri wa treni kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani - WFP katika stesheni ya mizigo Ilala jijini Dar es salaam tarehe 11 mwezi septemba 2023.

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema makasha ya ubaridi yaliyopokelewa yatasaidia wakulima na wafanyabiashara wa mbogamboga, matunda na samaki kusafirisha mazao katika mikoa ya Dar es salaam, Morogoro na Dodoma yakiwa katika hali safi kutoka shambani hadi sokoni.

"TRC kwa kushirikiana na WFP wamekuja na mradi wa kuwasaidia wakulima kwa kusafirisha mbogamboga na matunda kwa urahisi zaidi kwa kutumia mabehewa yenye makasha ya kuhifadhi ubaridi kwahiyo tumeandaa miundombinu ya kisasa kwaajili ya kusafirisha kutoka shambani hadi sokoni na hii itaongeza pato kwa wakulima, wafugaji na wavuvi"amesisitiza Prof. Mbarawa.

Pia Waziri Mbarawa ameongeza kua Wizara ya Uchukuzi itashirikiana na wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Viwanda kuunga mkono jitihada zinazofanywa kati ya TRC na WFP kuhakikisha upatikanaji wa masoko, miundombinu ya kuhifadhi mbogamboga na matunda pamoja na usafirishaji wa uhakika na gharama nafuu ili kuwezesha wakulima kupata na kuleta maendeleo katika nchi yetu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bi. Amina Lumuli amesema lengo ni kuhakikisha TRC inawafikia wakulima, wafugaji na wavuvi kwa kuwezesha kusafirisha mazao ya mbogamboga, nyama na samaki na hii itawezesha kuwaongezea kipato katika shughuli zao.

"TRC kama shirika la umma lipo tayari kuunga mkono sera za serikali katika kuwezesha wananchi kujiinua kiuchumi kupitia shughuli wanazofanya" ameongeza Bi. Amina.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli amesema makasha ya ubaridi yatasaidia wakulima wa mbogamboga na matunda kuendesha kilimo cha faida kwani watakua wanasafirisha mazao yao kwa usalama na kufika sokoni salama.

"Uboreshaji huu utaanzia mashambani hadi katika usafirishaji kwahiyo hii itampa faida mfanyabiashara wa mazao ya kilimo na mkulima”amesisitiza Katibu Mkuu Mweli.

Mkuu wa Kitengo cha Mnyororo wa Thamani WFP Bw. Mahamud Mabuyu amesema mradi umelenga kumsaidia mkulima hadi mfanyabiashara wa mazao kwa kuhakikisha kilichosafirishwa kinafika katika hali ya ubora.

"Mradi huu umegawanyika katika sehemu tatu ambazo ni wazalishaji, wasafirishaji na sokoni kwahiyo tumelenga kuweka muunganiko kati yao ili waweze kutoa kitu bora ikiwemo kupanga bidhaa katika hali inayofaa ikiwemo kupanga mazao na matunda kwa kupanga kila zao na kasha lake" ameongeza Mabuyu.

TRC na WFP ni mashirika ambayo yamekua yakifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa katika ukarabati na uboreshaji wa mabehewa ya mizigo ili kuwezesha usafirishaji wa mizigo na bidhaa mbalimbali kwa wafanyabiashara wanaotumia huduma ya reli kusafirisha mizigo.