Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

TRC YAPOKEA BEHEWA 14 MPYA ZA SGR KWAAJILI YA ABIRIA


news title here
25
November
2022

Shirika la Reli Tanzania – TRC limepokea behewa 14 mpya za reli ya kisasa - SGR zilizonunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwaajili ya uendeshaji wa reli ya kisasa nchini, hafla ya upokeaji wa behewa hizo imefayika katika bandari ya Dar es Salaam Novemba 25, 2022.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa reli ya kisasa - SGR unakwenda sambamba na ununuzi wa Behewa na vichwa vya treni kwaajili ya uendeshaji wa huduma katika reli ya kisasa. Ambapo leo Serikali ya Tanzania imepokea behewa za abiria 14 kati ya 59 zilizotengenezwa na kampuni ya Sun Shin Rolling Stock Technology Limited (SSRST) iliyopo nchini Korea ya Kusini.

Prof. Mbarawa ameongeza kuwa Serikali imetoa Dola za Marekani million 295.74 kwa kampuni ya Hyundai Rotem ya Korea Kusini kwaajili ya ununuzi wa vichwa vya treni vya umeme 17 na seti za treni za kisasa (Electric Multiple Unit - EMU) 10 na ‘locomotive simulator’ 1 ya umeme, pia kuna behewa 1,430 za mizigo ambazo ziko katika matengenezo.

Aidha, Prof. Mbarawa ametoa ufafanuzi kuhus aina ya treni zinazokuja nchini Tanzania, “Serikali imeagiza vichwa vya treni ya umeme kwaajili ya kuvuta behewa hizi, katika treni za umeme kuna vichwa vya treni aina 3 ambavyo ni ‘Electric Locomotive’ kazi yake ni kuvuta behewa kama hizi 14 zilizokuja, ‘Electric Multiple Unit’ (EMU kichwa cha treni ya aina hii kimeungwa na behewa pamoja, na aina ya tatu kichwa cha treni ni kile ambacho kinatumika mahususi kwa ajili ya mwendo kasi wa hali ya juu”.

Prof. Mbarawa ameweka wazi kuwa “kwenye utaratibu wa treni za umeme, treni inayokwenda mwendokasi zaidi ya Kilomita 200 kwa saatreni hiyo inaitwa ni ya mwendokasi, na zile treni ambazo mwendo wake ni chini ya Kilomita 200 kwa saa zinaitwa treni za kawaida. Hivyo treni yetu ya Tanzania ni treni ya umeme ya kawaida inayokwenda Kilomita 160 kwa saa”.

Balozi wa Korea Kusini nchini Tanzania Mhe. Kim Sun Pyo amesema leo ni siku ya historia kubwa kati ya Tanzania na Nchi yaKorea Kusini kwa kuleta behewa za SGR nchini Tanzania, Mhe. Kim amesisitiza kuwa Korea Kusini itaendelea kutoa ushirikianokatika kusaidia mradi wa SGR. Hata hivyo ametoa pongezi kwa Serikali na TRC kwa ujenzi wa SGR ambao utarahisisha usafirishaji na kuinua uchumi Tanzania.

Naye Mkurugenzi Mkuu TRC Masanja Kadogosa ameeleza gharama zilizotumika katika utengenezaji wa behewa hizo, “mkataba wa utengezaji wa Behewa hizi 59 ambazo behewa 14 tumezipokea leo umegharimu Dola za Kimarekani 55.6, muda wa mkataba ulikuwa miaka miwili ambao unahusisha utengenezaji wa behewa za daraja la juu (Business class) na daraja la chini (Economy class), kusafirisha, kufanya majaribio na mafunzo kwaajili ya wasimamizi wetu kupitia TRC. Kwa taarifa tulizonazo mpaka sasa utengenezaji wa behewa zilizobaki umefikia asilimia 86 na mwezi Mei 2023 tutakuwa tumepokea behewa zote 59”.

Sambamba na hivyo Kadogosa ameeleza mipango ya uboreshaji huduma za usafiri wa treni za bara katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka. Kadogosa amesema TRC kupitia Serikali imeongeza behewa 22 mpya za reli ya kati (MGR) ambazo zitasaidia kuongeza safari kwa za abiria wa kwa mikoa ya Kigoma ,Kilimanjaro na Arusha .