Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YALIPA FIDIA MKOANI DODOMA KUWEZESHA UJENZI WA VIVUKO SGR


news title here
09
June
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea na zoezi la ulipaji fidia Dodoma Jiji, Bahi, Chamwino na Mpwapwa katika kipande cha pili cha ujenzi wa reli ya kisasa Morogoro - Makutupora, Juni 2023.

Fidia zimelipwa kwa wananchi kwaajili ya kupisha maeneo yao kuwezesha ujenzi wa Vivuko, sehemu ya kuchimba kifusi na kumwaga kifusi kwenye mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa. Takribani wananchi 339 wamelipwa hundi zao na wengine wanaendelea kulipwa stahiki zao mkoani Dodoma.

Afisa Mtendaji wa Kijiji Cha Mnase Bi. Aksa Peter Mazengo wilaya ya Chamwino mkoa wa Dodoma amewapongeza wananchi wa kijiji cha Mnase kwa kuonesha ushirikiano mzuri kwa Serikali na TRC kupisha maeneo yao kwaajili ya kuwezesha ujenzi wa reli kuendelea katika mkoa wa Dodoma.

"Napenda kuwashauri wananchi waliolipwa fidia waende wakazitumie kununua mashamba na viwanja ili waweze kujenga na kuendelea na shughuli za kilimo na ufugaji kama ilivyokua awali kabla hawajapisha maeneo yao hapo awali" amesema Aksa Peter Mazengo.

Mhandisi ujenzi kutoka TRC Jacqueline Rusohoka ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Reli Tanzania kwa kuweza kuwalipa stahiki zao wananchi waliotwaliwa maeneo yao, pia amewashukuru wananchi wa Dodoma kufika kwa wakati kuchukua malipo ya fidia ili kupisha ujenzi wa vivuko vya magari na waenda kwa miguu katika reli ya kisasa SGR.