TRC YAIBUKA KIDEDEA TUZO UTUNZAJI MAZINGIRA

June
2025
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Philip Isdor Mpango amelikabidhi Shirika la Reli Tanzania (TRC), tuzo maalumu ya utunzaji mazingira kwa mwaka 2025,.
Makamu wa Rais, amekabidhi tuzo hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya Mazingira duniani iliyofanyika jijini Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Juni 05, 2025.
TRC imeshinda tuzo hiyo ikiwa ni miongoni mwa taasisi za serikali ambapo imeweza kutunza mazingira kwa kudhibiti uzalishaji wa gesi joto kiasi cha tani 16,571 ambayo ilikuwa ikizalishwa kupitia njia zingine za usafirishaji.
Licha ya kupunguza uzalishaji wa gesi joto mradi wa SGR pia umeweza kudhibiti uchafuzi wa kelele ( noise pollution) ,Msongamano wa watu na magari katika makutano ya barabara pia imelinda vyanzo vya maji na viumbe hai kwa kujenga madaraja makubwa na vivuko .
Akizungumza katika kilele hicho, Dkt. Mpango, amesema Tanzania imeunda mikakati madhubuti kupambana na uchafuzi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, upandaji miti, kupunguza uzalishaji wa matumizi ya plastiki na kufanya shughuli za uendeshaji hasa katika sekta ya usafirishaji na madini.
Mhe.Mpango ameongeza kuwa ni wakati wa Watanzania kuchukua hatua madhubuti za kuyalinda mazingira ili kuvilinda viumbe hai na uoto wa asilia kuepusha nchi kukumbwa na majanga kama njaa, mafuriko, jangwa, maporomoko ya milima na kutoweka kwa viumbe hai.
Katika hatua nyingine Naibu Mkurugenzi Mkuu (miundombinu) wa Shirika la Reli, Mhandisi Machibya Shiwa, akizungumzia tuzo hiyo, amesema Shirika la Reli Tanzania litaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuyalinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi kupitia usafirishaji.