Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAIBUKA KIDEDEA MAONESHO YA SABASABA 2023


news title here
14
July
2023

Shirika la Reli Tanzania – TRC laibuka kidedea kwa kushika nafasi ya kwanza katika Maonesho ya 47 ya kimataifa ya biashara maarufu SABASABA na kupata Tuzo katika sekta ya Usafirishaji nchini, wakati wa hafla ya kufunga maonesho jijini Dar es Salaam Julai 13, 2023.

TRC imeshiriki maonesho ya Sabasaba kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2023 yaliyofunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Julai 5, 2023. Lengo la maonesho ya Sabasaba ni kuwakutanisha wafanyabiashara, watoa huduma wa Sekta binafsi na Sekta ya umma pamoja na wateja.

Katika maonesho ya 47 TRC imeweza kuonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na Shirika ikiwemo utoaji wa huduma ya usafiri wa abiria na usafirishaji mizigo pamoja na miradi inayotekelezwa ukiwemo mradi wa reli yenye kiwango cha kimataifa (SGR). Aidha, wananchi waliotembelea banda la TRC walipata elimu kuhusu historia ya reli na namna Shirika linavyofanya kazi.

Kupitia weledi, kujituma na ufanisi katika maonesho TRC imeweza kutwaa ushindi huo ambapo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bw. Vicent Tangoh ameipongeza timu nzima iliyoshiriki katika maonesho ya Sabasaba na kuleta heshima kwa Shirika pamoja na sekta nzima ya usafirishaji Tanzania.

“Hii Tuzo imetuheshimisha sana wanaTRC pamoja na sekta ya usafirishaji nchini hasa usafirishaji kwa njia ya reli” alisema Bw. Tangoh.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano kutoka TRC Bi. Jamila Mbarouk ametoa shukurani kwa Mkrugenzi Mkuu wa TRC Ndugu Masanja Kadogosa kwa kuendelea kuwezesha wafanyakazi kufanya vizuri katika kila jambo analoelekeza.

“Tunafurahi TRC imeibuka kidedea na hii inaonesha ni jinsi gani timu nzima imeweza kushiriki katika maonesho ya Sabasaba kwa ufanisi, umoja hadi kupata ushindi” alisema Bi. Jamila.

TRC imeshinda tuzo ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ushiriki katika maonesho ya Sabasaba ambapo kwa miaka miwili mfululizo TRC imekuwa ikishinda nafasi ya pili.

TRC inaendelea vema kutoa huduma za usafirishaji wa mizigo na abiria kwa reli ya kati na kaskazini na kusimamia mradi wenye kiwango cha kimataifa (SGR) kwa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam - Mwanza na awamu ya pili Tabora-Kigoma.