Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAHUDHURIA KONGAMANO LA UWT LA MIAKA MIWILI YA RAIS SAMIA


news title here
20
March
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limejumuika katika kusherekea miaka miwili ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt Samia Hassan Suluhu katika uwanja wa uhuru, jijini Dar es Salaam Machi 19, 2023.

UWT wameandaa kongamano kwa lengo la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za utendaji wake katika nyanja zote muhimu kwa muda wa miaka miwili tangu ashike nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Raisi Samia amesema hakuna mradi uliosimama kutekelezwa tangu amechukua madaraka ya Urais Machi 2021 katika nyanja zote ikiwemo sekta ya Maji, Usafirishaji na Elimu vyote vinaendelea vizuri.

Ameongeza kuwa, kupitia kaulimbiu ya wanawake 2023 Teknolojia na ubunifu ndio msingi wa maendeleo, kupitia teknolojia Serikali imeweza kujenga miundombinu kwa urahisi ikiwemo ujenzi wa barabara, reli, miradi ya maji na bandari.

Katibu Mkuu wa UWT Taifa Dk. Philis Nyimbi amesema katika kusherekea miaka ya miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan Tanzania imeshuhudia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ukiendelea katika vipande vinne ambavyo ni Morogoro - Makutupora, Makutupora - Tabora, Tabora - Isaka pamoja na Isaka - Mwanza.

"Tunaona miundombinu ya reli, barabara imeimarika na ujenzi wa madaraja yenye viwango kuanzia vijijini Hadi mijini." ameongeza Dk. Philis.

Mhandisi wa Ishara na Mawasiliano TRC Farida Njoka ameishukuru UWT kwa kuialika TRC kuhudhuria kongamano la miaka miwili ya Dkt. Samia Suluhu kwani TRC imeguswa na Rais Dkt. Samia Suluhu katika ujenzi wa miundombinu ya reli pamoja na ununuzi wa mabehewa mapya za reli ya kati – MGR na mabehewa mapya za SGR.

"Tuna Imani na uongozi wa Rais Samia kwani kupitia yeye TRC inaenda kuiunganisha Tanzania kibiashara na nchi jirani zikiwemo DRC, Burundi, Kenya na Uganda kupitia reli ya kisasa pindi tu ujenzi ukikamilika, vilevile kupitia reli tunaenda kurahisisha usafirishaji mizigo na kuokoa muda pia itasaidia kuzuia uharibifu wa miundombinu ya barabara kwani malori yatapungua barabarani," ameongeza Mhandisi Farida.