TRC YAHITIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

October
2024
Shirika la Reli Tanzania – TRC limehitimisha wiki ya huduma kwa wateja katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora, Kigoma na Kilimanjaro iliyoadhimishwa kuanzia tarehe 7 hadi 11 Oktoba 2024.
Wiki ya huduma kwa wateja mwaka 2024 imebeba ujumbe unaosema ‘ABOVE AND BEYOND’ ukimaanisha huduma bora zaidi. Lengo la wiki ya huduma kwa wateja ni kutathimini kiwango cha huduma kwa wateja pamoja na mchango wa wateja katika ustawi wa taasisi ili kuboresha mazingira ya utoaji huduma na viwango vya ubora katika huduma.
TRC imeadhimishwa Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kushirikiana na kampuni ya TIGO Tanzania na SMH Rail ikiwa ni sehemu ya wadau wanaoshirikiana na TRC katika kuboresha utoaji wa huduma za usafiri wa reli nchini.
“TRC inashirikiana na TIGO katika kutambua na kuthamini mchango wa wateja katika ustawi wa taasisi hizi mbili. TIGO imekuwa na nafasi kubwa katika huduma za Tiketi Mtandao ambapo abiria wanaweza kufanya malipo kwa urahisi bila ya kuwepo na urasimu, hii inaleta thamani kwenye huduma zetu. Pia kampuni ya SMH Rail imekuwa mdau mkubwa katika uboreshaji wa huduma kupitia kazi ya ukarabati wa vitendea kazi ikiwemo vichwa vya treni pamoja na kutoa ushauri wa namna bora ya kuboresha vitendea kazi” alieleza Kadogosa
Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kadogosa alisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya reli nchini ni matokeo ya wateja waaminifu ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa kodi ambazo zimewezesha kuimarisha sekta ya reli nchini.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TRC Bi. Amina Lumuli wakati wa kufunga wiki ya huduma kwa wateja jijini Dodoma alisema kuwa wiki ya huduma kwa wateja inakumbusha majukumu muhimu yanayotekelezwa na Shirika la Reli Tanzania, pia ilikuwa wiki ya sherehe kwa kila mmoja kwa kazi nzuri zinazofanywa kila siku katika kutimiza mahitaji ya wateja.
Katika wiki ya huduma kwa wateja TRC iliweza kutambua mchango wa wadau mbalimbali kwa kutoa zawadi kwaajili ya kuthamini juhudi zao katika utoaji huduma. Miongoni mwa waliopewa zawadi ni pamoja na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kuanza kwa huduma za treni za mwendokasi, Mkurugenzi Mkuu TRC Masanja Kadogosa, Wadau kampuni ya TIGO na SMH Rail Pamoja na Wafanyakazi bora ambao walipatikana kwa kupigiwa kura kama watumishi wanaotoa huduma bora zaidi kwa wateja.