Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAFUNGUA WIKI YA USALAMA WA RELI TANZANIA


news title here
11
October
2022

Shirika la Reli Tanzania – TRC yafungua wiki ya usalama wa reli ambayo huadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 10 hadi 13 mwezi Oktoba. Ufunguzi wa wiki ya usalama umefunguliwa na mgeni rasmi Naibu Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini - LATRA katika ukumbi wa jengo la Stesheni ya Dar es Salaam Oktoba 10, 2022.

Maadhimisho haya hufanyika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kupitia Vyama vya Reli Kusini mwa Afrika – SARA yaani South African Railway Association. Maadhimisho huwa na kauli mbiu tofauti kila mwaka, kwa mwaka 2022 kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “CHUKUA TAHADHARİ, TRENİ ZİNA MWENDO WA HARAKA, NI HATARI”.

Wiki ya Usalama wa Reli huambatana na utoaji elimu ya masuala ya usalama wa reli kwa watumiaji wa usafiri wa reli, wananchi na wadau kupitia vyombo vya habari na mikutano ya wananchi ili kuhakikisha miundombinu ya reli na jamii inakuwa salama. Utoaji elimu unalenga kutoa uelewa kuhusu usalama kwenye maeneo ya reli, ulinzi wa miundombinu ya reli, na kuwakumbusha watumiaji wa barabara kuchukua tahadhari wanapokatiza miundombinu ya reli.

Katika kuadhimisha Wiki ya Usalama wa Reli, Mwenyekiti wa Bodi LATRA amewasisitiza wafanyakazi wa TRC kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia Sheria na kanuni za reli kwa kuhakikisha usalama wa njia ya reli, behewa na vichwa vya treni ili kuhakikisha usalama wa abiria na mali za wateja wa TRC.

Pia amewataka wafanyakazi wa TRC kua mabalozi wazuri kwa wananchi wanaoishi jirani na reli na wanaofanya shughuli za kijamii karibu na reli kwa kuzingatia usalama wao pamoja na usalama wa reli kwa kufuata alama za usalama wa reli.

“Behewa zote zifanyiwe matengenezo kabla ya safari kuanza ili kuhakikisha usalama muda wote wa safari pindi treni iwapo safarini ili kuzuia ajali na uharibifu wa mabehewa na miundombinu pamoja na maisha ya watu na mali zao”ameongeza Henry Mgalla.

Ameongeza Shirika la Reli linafanya kazi kwa kutumia sheria ya reli nchini ambayo ni namba 10 ya mwaka 2017 na kanuni ndogo za reli, TRC inazingatia Sheria ya reli katika kuhakikisha usalama wa miundombinu ya reli pamoja na usafirishaji wa abiria na mizigo.

Aidha, Mkurugenzi amewataka madereva wazingatie alama za usalama katika makutano ya reli na barabara na kutovuka reli bila kuruhusiwa na askari au mshika bendera kwenye makutano ya reli na barabara vilevile kuacha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya reli.

Naye Bwana Benjamini Mbimbi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi amesema usalama wa reli ni jukumu la kila mmoja ili kuepusha ajali zinazoepukika vilevile amesistiza wananchi kufuata utaratibu na Sheria za reli wawapo maeneo ya reli.

“Zoezi hili la wiki ya usalama wa reli litakua linafanyika kila mwaka nchini Tanzania kwa wafanyakazi na wananchi ili kukumbushana mazingatio ya usalama wa reli pindi tuwapo kazini na pindi tutumiapo usafiri wa reli nchini’’ Benjamin Mbimbi