TRC YAFANYA KIKAO CHA MWISHO CHA BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI

October
2021
Shirika la Reli Tanzania - TRC limefanya kikao cha mwisho cha Baraza Kuu la Wafanyakazi kwa lengo la kutathimini mambo yaliyofanyika katika shirika ili kuzidi kuboresha ufanisi wa kazi
, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa City Garden jijini Dar es Salaam, Oktoba 2021.
Mkurugenzi Mkuu TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa ameeleza kuwa kupitia baraza hilo wawakilishi wa wafanyakazi wameweza kutathimini ndani ya miaka mitatu Shirika limeweza kufanikiwa kwa kiasi gani kwa kufikia malengo ya mipango iliyowekwa katika kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kufungua reli ya kaskazini, ujenzi wa reli ya kisasa - SGR na kuboresha huduma kupitia mifumo ya kielektroniki.
Ndugu Kadogosa amesema kuwa Baraza hilo ni chombo muhimu kwa kuwashirikisha wafanyakazi katika mambo yanayotokea kwenye taasisi ili kuweza kuboresha ufanisi katika kazi.
“Wafanyakazi ndio watekelezaji, wanapaswa kujua dira ya taasisi inapoenda na kushirikishwa kwenye mambo yanayotokea katika taasisi” alisema Ndugu Kadogosa.
Aidha, Ndugu Kadogosa ameeleza kuwa TRC ni kubwa sana na ipo katika maeneo mbalimbali kama Kigoma, Mpanda , Moshi, Arusha, Morogoro, Tabora , Mwanza hivyo wawakilishi hao watafikisha mambo na maamuzi yaliyojadiliwa katika maeneo yote ya reli kwa maslahi ya wafanyakazi.
“Katika utendaji lazima watu wapate ujumbe, baraza ndilo linalopeleka uelekeo wa taasisi nchi nzima ili wafanyakazi kujua kinachoendelea na pia kuleta utulivu katika ufanyaji kazi” alieleza Ndugu Kadogosa
”TRC tupo zaidi wa wafanyakazi elfu tatu wa taasisi lakini tukijumlisha na wale wa njia ni zaidi ya wafanyakazi elf ishirini“ aliongezea.
Hata hivyo Kadogosa amesema kuwa kwa mujibu wa sheria taasisi zote za serikali lazima ziwe na baraza la wafanyakazi hivyo wanatarajia kuchagua wajumbe wengine wa baraza jipya lijalo watakaobeba mambo ya kitaasisi kwa maslahi ya wafanyakazi.
Naye mjumbe mwakilishi kutoka Chama Cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania - TRAWU mkoani Morogoro Bi. Asia Bakari amesema kuwa baraza hilo la wafanyakazi lina umuhimu mkubwa katika shirika kwa wafanyakazi na menejimenti kuweza kupanga mikakati ya maendeleo ya jumla kwa shirika zima pamoja na maendeleo ya wafanyakazi pamoja na kuimarisha taifa.
“Baraza hili limekuwa kiungo kikubwa sana kwa wafanyakazi na menejimenti kwa kuweza kusimamia pamoja muendelezo wa shirika letu, kulinda rasilimali zetu , pamoja na kuboresha maslahi ya wafanyakazi na shirika” alisema Bi. Asia.
Mwakalishi wa baraza la wafanyakazi kutoka Mpanda Bw. Athumani Saidi ametoa shukrani kwa menejimenti ya TRC na Baraza kuweza kusimamia na kutekeleza kile kinachojadiliwa ndani ya baraza hilo ili kuzidisha ufanisi na kuboresha utendaji wa kazi kwa wafanyakazi katika taasisi.