TRC YAENDELEA NA ZOEZI LA UTWAAJI ARDHI MKOANI SHINYANGA

September
2022
TRC imefanya zoezi la uhamishaji makaburi katika vijiji vya Didia, Sumbigu, Ishololo, Puni, Nyashimbi, Zobogo, Bunonga na Sumbigu Wilaya ya Shinyanga vijijini Septemba 2022.
Zoezi hilo lina lengo la kutwaa maeneo kwaajili ya kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ikiwemo eneo la kumwaga kifusi pamoja na kuchimba kifusi katika kipande cha tano Isaka - Mwanza.
Mhandisi kutoka TRC Oliver Julius amewashukuru wananchi pamoja na viongozi wa vijiji kwa kutoa ushirikiano mzuri wa zoezi hilo la kuhamisha miili ya wapendwa wao kwenye vijiji hivyo.
"Tumetoa elimu ya uhamishaji makaburi katika vijiji vya Didia, Bunonga, Zobogo, Mwamanyuda, Ishololo, Puni, Nyashimbi, Sumbingu na Bunonga" alisema Mhandisi Julius.
Afisa Afya wa Kata ya Didia Wilaya ya Shinyanga vijijini Bi. Eduardina Maganga amesema watu wa Afya wanahakikisha usalama wa wachimbaji, wazikaji pamoja na wafanyakazi wote wanaohusika na zoezi la uhamishaji wa makaburi kwa kuwapa vitendea kazi ikiwemo mipira ya kuvaa mikononi, barakoa na Dawa za kuwalinda dhidi ya magonjwa yaambukizayo.
"TRC imefanya jambo zuri kuweza kutushirikisha watu wa Afya kwenye hili zoezi kwani tunaweza kuhifadhi mabaki ya miili kwa usalama zaidi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za afya katika zoezi la uhamishaji wa miili, " Bi Eduardina Maganga.
Mkazi wa Kijiji cha Bunonga Mzee Mayila ameishukuru TRC kwa kuandaa zoezi kiuadilifu pamoja na Serikali ya Kijiji kwa kutoa eneo la kuhifadhia wapendwa wao.