Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA NA ZOEZI LA ULIPAJI FIDIA MKOANI MOROGORO


news title here
14
August
2023

Shirika la Reli Tanzania - TRC limeendelea na zoezi la kulipa fidia kwa wananchi waliopisha maeneo yao kufanikisha ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa katika kipande cha kwanza Dar es Salaam - Morogoro mwezi Agosti 2023.

Wananchi 21 wamelipwa fidia na wengine wanaendelea kulipwa katika Kijiji cha Mtego wa Simba na Yespa, wananchi wamepisha njia ya umeme na maeneo ya nyongeza kwaajili ya kumuwezesha mkandarasi kuendelea na ujenzi wa miundombinu katika eneo ambako mradi umepita.

Afisa Jamii kutoka TRC Bi. Catherine Mwakagali amesema timu kutoka TRC imefanikiwa kulipa fidia wananchi waliopitiwa na mradi kwa kutoa eneo lililokua na makaburi baada ya kufanya zoezi la uhamishaji wa miili na zoezi la ulipaji limeenda vizuri katika ofisi za vijiji.

"Tunashukuru kwa Ushirikiano wa wananchi wote waliotwaliwa ardhi na viongozi wa vijiji ambao ni wenyeviti na Maafisa watendaji ambao walionesha ushirikiano mzuri tangu mwanzo wa zoezi la utwaaji ardhi hadi Sasa tulipofikia malipo ya hundi kwa wananchi" ameongeza Bi Catherine.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mtego wa Simba Bwana Mohamed Mbega amewapongeza wananchi kwa kuweza kufika na nyaraka muhimu zote za kuwezesha kupokea hundi ikiwemo vitambulisho, picha na nyaraka za uthamini ambazo walitakiwa kufika nazo katika ofisi ya serikali ya kijiji.

"Pia niipongeze timu nzima ya TRC ilivyoweza kufika kwa wakati na kuweza kufanikisha zoezi hili kwa muda uliopangwa" ameongeza Mbega.