TRC YAENDELEA NA ZOEZI LA ULIPAJI FIDIA KWA WANANCHI MKOANI MOROGORO

August
2021
Shirika la Reli Tanzania - TRC linaendelea kuwanufaisha wananchi mkoani Morogoro kufuatia zoezi endelevu la ulipaji wa fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao kupisha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa - SGR kipande cha Dar es Salaam - Morogoro lililofanyika katika eneo la Mikese mjini na ofisi ya kata ya Tangi la maji hivi karibuni, Agosti 2021.
Malipo hayo ya fidia yanaendelea kutokana kwa wananchi ambao walipata changakoto mbalimbali za nyaraka zao ambazo kwa sasa zimekamilika ikiwemo kutokuwa na picha kwenye jeduari husika la malipo, majina kutofautiana wakati wa uthamini pamoja migogoro ya mirathi.
Mkaguzi majengo kutoka TRC Bw. Ramadhan Mfikilwa amesema kuwa wananchi wanaendelea kutoa ushirikiano wa kutoa maeneo yao ambayo tayari yametwaliwa na kuwa tayari kusubiri malipo yao pindi yanapokuwa tayari.
“Wananchi wanaendelea kutoa ushirikiano toka mwanzo tuko pamoja nao hadi sasa tulipofikia” alisema Bw. Ramadhan.
Naye mtendaji wa Mikese mjini Bw. Haji Maridadi ameishukuru serikali kwa kuendelea kulipa fidia kwa wananchi ambao hawakupata stahiki zao ili kuepusha migogoro katika maeneo yao na kuwaaminisha kuwa kila mtu ana haki ya kupatiwa fidia endapo eneo lake litatwaliwa.
Hata hivyo Bw. Maridadi ametoa rai kwa wananchi kuwa wepesi wa kuitikia wito katika mambo mbalimbali yanayohusiana na mradi wa SGR ili kukubaliana kwa haraka pindi maeneo yanapohitajika kwa kufuata taratibu zote za malipo ili kupisha shughuli za ujenzi.
Zoezi la ulipaji wa fidia ni zoezi endelevu kwa wananchi katika maeneo yanayotwaliwa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa SGR hadi mradi huo utakapokamilika na kuanza uendeshaji.