Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Shirika la Reli Tanzania

​TRC YAENDELEA NA ZOEZI LA ULIPAJI FIDIA KUWEZESHA UJENZI WA SGR MKOANI DODOMA


news title here
06
April
2023

Shirika la Reli - TRC limeendelea na zoezi la ulipaji fidia mkoani dodoma kwa wananchi waliotwaliwa ardhi zao katika wilaya ya Bahi, Dodoma jiji, Chamwino na Mpwapwa katika kipande cha pili Morogoro - Makutupora cha ujenzi wa reli ya kisasa, April 2023.

Wananchi wamelipwa fidia kupisha maeneo kwaajili ya kumuwezesha mkandarasi kupata maeneo ya kumwaga kifusi, ujenzi wa vivuko pamoja na maeneo ya kuchukua udongo kwaajili ya ujenzi wa SGR.

Mthamini Bi. Lulu Lyimo kutoka TRC amewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi wakati wa malipo ya fidia na amewashukuru kwa kuendelea kuiamini TRC na kuendelea kujitolea maeneo yao kwaajili ya kupisha shughuli za ujenzi wa miundombinu ya reli ya kiwango cha kimataifa katika mkoa wa Dodoma.

Wananchi wa vijiji 18 katika wilaya ya Bahi, Dodoma Jiji, Chamwino na Mpwapwa wanaendelea kulipwa fidia mkoani Dodoma.

Wananchi wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na TRC kwa kuweza kuwalipa stahiki zao na kuwapa elimu wakati wa utwaaji ardhi kwa kuzingatia Sheria za Ardhi wakati wa uthamini.

Zoezi la utwaaji ardhi na ulipaji fidia ni endelevu kwa Shirika la Reli Tanzania na linakwenda sambamba na utekelezaji wa mradi kwasababu mradi wa SGR ni sanifu jenga, hivyo ardhi hutwaliwa kutokana na mahitaji ya Mkandarasi wa mradi kulingana na usanifu na mahitaji ya ujenzi kwa wakati na eneo husika katika maeneo yote inakopita reli ya SGR nchini.